WAHADHIRI takriban 800 waliopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameazimia kutoingia madarasani kufundisha kuanzia Novemba 2 mwaka huu mpaka hapo serikali itakaposhughulikia suala la muundo mpya wa mishahara.
Kauli
hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma wa UDOM
(Udomasa), Gerald Shija alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu maazimio ya mkutano mkuu wa wanataaluma hao uliofanyika Septemba
21 mwaka huu.
Amesema kwa pamoja wameazimia na kutoa msimamo huo mpaka hapo serikali itakapotekeleza.
Kwa
mujibu wa Shija alidai kuwa Rais alitoa taarifa kupitia vyombo vya
habari Agosti 22 mwaka 2013 ambao uliagiza muundo huo uanze kutumika
Julai Mosi mwaka huu lakini mpaka sasa haujaanza.
Amesema
kumekuwepo na mishahara isiyofanana kwa watu wenye elimu inayofanana na
kufanya kazi inayofanana na hivyo kutofautiana na sera ya Serikali
inayoelekeza kuwa watu wenye elimu inayofanana kulipwa mishahara
inayofanana.
Shija
amesema wanaamini kuwa muundo huo wa utumishi ulioanishwa na
wanataaluma ndio muundo bora ukilinganisha na muundo unaotumika sasa
hivi.
Aliiomba
serikali kutekeleza muundo huo ili kuondoa kero ambazo zilibainishwa
kwa Rais, hali iliyomfanya aagize uanzishwaji na utekelezwaji wa muundo
huo.
Aidha
amesema hivi sasa hawana imani na viongozi wa serikali kutokana na
kutotekeleza muundo huo katika kutatua kero za muundo uliopo hivi sasa.
“Ucheweleshwaji
wa muundo huu umekuwa ukikwamishwa na Hazina, Chuo Kikuu cha Dodoma
pamoja na Utumishi wa umma ambapo wamekuwa wakitupiana mpira,” amesema Shija.
Hata
hivyo amesema mnamo Desemba 11, 2014, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilitoa
waraka kuagiza Vyuo kupitia Ofisi za rasilimali watu kuzingatia
utaratibu ulioanishwa katika muundo na wanataaluma ikiwemo masuala ya
vyeo na kuajiri kwakuzingatia vigezo na kuwapanga watumishi wanataaluma.
Naye
Katibu Mkuu wa Umoja huo, Lameck Thomas amesema kuwa muundo huo
ulilenga kuweka usawa wa maslahi ya watendaji wa Vyuo vikuu na Vyuo vya
Umma na vyuo vikuu vishiriki ili wawe sawa lakini hakuna
kilichotekelezwa.
“Kwa
kweli nieleze kwa masikitiko makubwa na tusingependa tufikie hatua hii
lakini serikali ndio imetufanya tufikie hapa, tutahakikisha tunapigania
muundo huu hadi tupate haki zetu kwani ni nyenzo sahihi lakini tatizo la
kulipwa mishahara tofauti kwa wahadhiri lipo katika Chuo Kikuu cha
Dodoma tofauti na vyuo vingine,” amesema Thomas.
Kwa
upande wake, Mjumbe wa Kamati Utendaji ya Udomasa, Mandela Peter
amesema bora muundo huo uje ili kuleta usawa kutokana na kutofautiana
kwa kiasi kikubwa mishahara kwa wahadhiri wa UDOM na vyuo vingine kama
vile Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
“Yaani
ukiangalia katika vyuo vya UDSM, Sokoine, Mzumbe ukilinganisha na UDOM
kuna tofauti kubwa kati ya Sh. 700,000 hadi 1,000,000 kwa mshahara
anaopokea mhadhiri msaidizi, sasa hapo utaona kutokana na tofauti hiyo
ni bora muundo huu uanze kutekelezwa ili tuwe sawa,” amesema Mandela.
Aidha
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania
(THTU) katika chuo hicho, Nashon Maisori aliiomba serikali kutopuuza
madai hao kwani wasipoyapatia ufumbuzi watasababisha zaidi ya wanafunzi
18,000 kuathirika kutokana na hali hiyo.