Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema asilimia 60 ya uvunjifu wa haki za binadamu nchini unafanywa na vyombo vya dola huku asilimia 40 ukifanywa na wananchi wa kawaida.
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba amesema kumekuwa na matukio ya
wananchi kuuawa wakiwa mikononi mwa askari polisi ambao kwa mujibu wa
sheria za kuundwa kwake ni walinzi wa raia na mali zao.
Akizungumza
katika maadhimisho ya miaka 20 ya kituo hicho, Bisimba amesema wananchi
wamepoteza uwoga kwa vyombo vya dola jambo linalopelekea kuvamia vituo
vya polisi mara kwa mara, kuwatoa mahabusu, kuua polisi na kupora
silaha.
Alitolea
mfano mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge mkoani
Morogoro yaliyotokea Januari 14, 2006 katika msitu wa Pande pembezoni
mwa Jiji la Dar es Salaam ambapo Sabinus Chigumbi (Jongo), Ephrahim
Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva wa teksi Juma Ndugu waliuawa.
“Pia
kumekuwa na vitisho na kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari
vinavyoandika habari za kuikosoa serikali kama ambavyo magazeti ya
Mwanahalisi, Mwananchi na The East African yalivyokumbwa na rungu la
serikali” alisema.
Jaji
Rufaa Mstaafu, Eusebia Munuo aliyekuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo
alisema sherehe hizo zimekuja sambamba na uchaguzi mkuu wa Tanzania na
kukitaka kituo hicho kuhamasisha makundi yote kupiga kura.
“Kama
mlivyohamasisha wakati wa zoezi la kujiandikisha, naomba muwahamasishe
wananchi kutumia haki yao ya kupigakura na kuchagua kiongozi wanayemtaka
na kujiepusha na vitendo vyovyote vya vurugu” alisema na kuongeza.
“Najua kituo hiki kinaheshimika na kwamba kina nguvu kubwa. Nina hakika wananchi watawasikiliza.”alisema Mmari
Mwenyekiti
wa bodi ya LHRC, Geoffrey Mmari alizindua kitabu kinachoelezea
changamoto za kituo tangu kilipoanzishwa hadi sasa, mafanikio
yaliyopatikana na uhusiano wake na vituo vingine.
Mmari
alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni Usalama wa wafanyakazi wa
kituo hicho, Vitisho, kigeugeu cha wateja na kituo kutegemea wafadhili.