Akizungumza
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage,
Shinyanga jana, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alimshukia Lowassa
akisema mradi wa kusambaza maji kutoka Ziwa Victoria ulianza miaka mingi
na kusimamiwa na Serikali ya Tanzania na Uholanzi wakati huo Lowassa,
ambaye alikuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo wakati wa
utekelezaji wake, alikuwa bado mwanafunzi.
Sitta
alisema katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu mradi huo ndipo
ulianza kusimamiwa na Serikali ya Tanzania chini ya mawaziri mbalimbali.
“Si Lowassa pekee aliyesimamia na kuanzisha mradi huu,” alisema Sitta.
“Sasa
mbona akisimama jukwaani anajitaja mwenyewe tu, mbona hawataji wenzake.
Nawaambieni ndugu zangu viongozi wanaopenda kujikweza kama hawa
waogopeni,” alisema Sitta na kushangiliwa.
Dk
Magufuli naye alichangia hoja hiyo wakati akijinadi aliposema kuwa
mradi huo, ambao umesaidia wakazi wengi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kupata
maji, ulianzishwa na kusimamiwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na si
Lowassa.
Dk
Magufuli, ambaye anajinadi kwa kutumia mafanikio ya ujenzi wa barabara,
alisema Lowassa ni mmoja wa mawaziri waliosimamia mradi huo na si yeye
aliyeubuni na kuuanzisha kama anavyojinadi katika mikutano yake ya
kampeni.
Tangu
kuanza kwa kampeni, Lowassa amewaahidi wananchi wa Kigoma, Bariadi na
Chato kuwa akiwa, rais atahakikisha wanapata maji kutoka Ziwa Victoria,
akieleza kuwa kama aliweza kufanikisha mradi wa maji kutoka ziwa hilo
kwenda Shinyanga, hawezi kushindwa katika maeneo hayo.
Lowassa alipokuwa Shinyanga, pia aliwaahidi wananchi wa mkoa huo kuwa akiwa rais watapata maji kutoka ziwa hilo.
Akijinadi
kwenye mkutano huo, Dk Magufuli alisema amejenga barabara nyingi akiwa
Waziri wa Ujenzi lakini hawezi kujisifu kuwa yeye ndiye aliyezijenga.
“Siwezi
kujisifu kwa kujenga barabara zaidi ya kilomita 17,000 wakati nikiwa
waziri wa ujenzi kwa miaka 15 katika Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne.
Huwezi kuwa na mtoto ukamtuma shambani akachume pamba kisha azilete na
kujisifu kuwa zile pamba ni zake,” alisema.
“Eti anasema alileta shule za kata. Hivi alibeba matofali kichwani wakati wa ujenzi wa shule hizi,” alihoji Dk Magufuli akimponda Lowassa ambaye pia, alisimamia ujenzi wa shule za kata wakati akiwa Waziri Mkuu.
Dk
Magufuli alisema akiwa rais, atahakikisha kata zote zisizo na maji
katika mji wa Shinyanga zinapata maji, huku akisisitiza kuwa maendeleo
ni changamoto na kwamba haziwezi kuisha zote.
Waziri
huyo wa Ujenzi aliahidi kujenga kilomita 10 za lami katika mji wa
Shinyanga mbali na kimomita 32 zilizojengwa mpaka sasa, ujenzi wa soko
la kisasa, chuo kikuu cha madini, kufuta ushuru kwa wakulima na
kuanzisha viwanda kwa kuhusisha sekta binafsi.
“Shinyanga
kuna kero ya kiwanda cha nyama ambacho kinasuasa mpaka kinatia
kichefuchefu. Siku nikiapishwa kuwa rais, mwenye kiwanda hiki aidha
kifanye kazi au kirejeshwe serikalini,” alisema na kushangiliwa na maelfu ya wananchi.
Alisema ni aibu kwa Watanzania kuwa maskini katika nchi yenye kila aina ya rasilimali.