RAIS Jakaya Kikwete amemwambia Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Angel Merkel, kuwa upo uhuru mkubwa na usiokuwa kifani kwa vyama vyote ya siasa kufanya kampeni zake kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Aidha,
Rais Kikwete amemwambia Kansela Merkel kuwa Jopo la Watu Mashuhuri
Duniani linalotafuta mapendekezo ya jinsi dunia inavyoweza kujiandaa
vizuri zaidi kwa magonjwa ya milipuko, sasa linakaribia kumaliza kazi
yake na lipo katika hatua ya kuandaa mapendekezo kuhusu nini dunia
ifanye katika siku zijazo.
Rais
Kikwete amesema hayo alipokutana na kuzungumza na Kansela Merkel,
katika mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Ujerumani kwenye Umoja wa
Mataifa (UN) mjini New York, ambako viongozi hao walikuwa na mazungumzo
ya ana kwa ana.
Viongozi
hao wawili wapo New York, Marekani kuhudhuria shughuli za mwaka huu za
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (United Nations General Assembly (UNGA).
Katika mazungumzo hayo, Kansela Merkel alitaka kujua kutoka kwa Rais
Kikwete kuhusu mwenendo mzima wa kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea
nchini na uhuru unaotolewa kwa kila chama kufanya kampeni zake.
“Kama
unavyojua Mheshimiwa Kansela tuko katikati ya Kampeni ya Uchaguzi Mkuu.
Kampeni zinakwenda vizuri. Tunao wagombea wa urais nadhani kiasi cha
wanane hivi na kila chama kinaendesha kampeni zake kwa uhuru mkubwa na
usiokuwa na kifani.
“Tunataka
mchakato ambao utazaa uchaguzi huru na wa haki na hivyo ni muhimu kwa
kila chama kuendesha shughuli zake za kampeni kwa uhuru,” alisema Rais Kikwete katika mazungumzo hayo.
Rais
pia amemwambia Kansela Merkel kuhusu baadhi ya mambo makubwa ya kampeni
yakiwemo yanayohusu masuala ya huduma za kijamii kama vile afya, elimu
na mapambano dhidi ya umasikini.
Rais
Kikwete pia ametumia mkutano wake na Kansela Merkel kumweleza mama huyo
kuhusu kazi ya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani kuhusu Matatizo ya Afya,
akisisitiza kuwa baada ya hatua ya kuwasikiliza watu mbali mbali, sasa
jopo limeanza kuandaa maoni yake na mapendekezo.
Jopo
hilo lililoteuliwa Aprili mwaka huu na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon
baada ya kutokea majonzi makubwa yaliyosababishwa na ugonjwa wa ebola
katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone, linatarajiwa kukabidhi
ripoti yake kwa Ban Ki-moon Desemba mwaka huu.