TEMEKE YAANZA AIRTEL RISING STARS KWA KISHINDO - LEKULE

Breaking

15 Sept 2015

TEMEKE YAANZA AIRTEL RISING STARS KWA KISHINDO


1
Mshambuliaji wa timu ya wasichana wa Temeke Christina Daudi (kushoto) akimtoka beki wa Arusha Vailet Valerian wakati timu hizo zilipokutana katika ufunguzi wa michuano ya Airtel Rising Stars kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini  Dar es Salaam Temeke walishinda magoli 8-0.
2
Mchezaji wa timu ya wasichana wa Temeke Madelin Enock (kushoto) akiwania mpira na mchezaji wa Arusha Mariam Rashid wakati timu hizo zilipokutana katika ufunguzi wa michuano ya Airtel Rising Stars kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaa jana. Temeke walishinda magoli 8-0.
3
Beki wa timu ya wasichana wa Temeke Eva Wailes, akiwatoka wachezaji wa Arusha wakati timu hizo zilipokutana katika ufunguzi wa michuano ya Airtel Rising Stars kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana. Temeke walishinda magoli 8-0.
Pazia la michuano Taifa ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars jana lilifunguliwa katika uwanja wa Kukumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam ambapo timu ya wasichana ya Temeke ilitoa onyo kali kwa timu shiriki kwa kuifunga Arusha 8-0.
Mchezo huo ulifuatiwa na mechi ya wavulana kati ya Mwanza na Kinondoni na Mwanza kuibuka na ushindi wa goli 1-0. Goli la Mwanza lilifungwa na Lazaro Richard katika dakika ya 42 kufuatia krosi iliyopigwa kutoka upande wa kushoto.
Katika mchezo wa kwanza, Temeke walianza kwa kasi ya aina yake na kupeleka mashambuliazi ya mara kwa mara langoni mwa Arusha huku Arusha wakionekana kuzidiwa katika kila idara.
Temeke waliandika bao la kwanza kupitia kwa Oppah Clement kaika dakika ya 24, baada ya kuwahadaa mabeki wa Arusha na kuachia shuti kali ambalo lilimshinda kipa wa Arusha.
Temeke awalipata bao lao la pili kupitia kwa Rose Mpoma mnamo dakika ya 27 ambaye aligongeana mpira kwa uzuri na Oppah Clement na kisha kumchambua kipa wa Arusha kwa umaridadi wa hali ya juu na kuukwamisha mpira huo kimiani.
Alikuwa ni Oppah Clement tena, ambaye aliiandikia Temeka bao la tatu mnamo dakika ya 28 baada ya kuunganisha krosi iliyochongwa na Shamimu Hamisi kutoka upande wa kushoto mwa uwanja na kuendeleza karamu ya magoli kwa Temeke.
Shamimu Hamisi aliifungia Temeke bao la nne katika dakika ya 51 na kuzidi kuzamisha jahazi la Arusha ambao walinekana kama vile wamesimama wakati mchezo ukiendelea.
Rosea Mpoma aliwaliza kwa mara nyingine tena Arusha baada ya kuifungia Temeke bao la tano katika dakika ya 53 baada ya kuachia shuti kali na kuzama moja kwa moja wavuni.
Temeke waliendeleza kupeleka kilio kwa Arusha baada ya Asia Juma kufunga goli la sita na la saba baada ya kuwatoka mabeki wa Arusha kwa nyakati tofauti na kuwapa raha mshabiki wao.
Shamimu Hamisi alihitimisha karamu ya magoli kwa Temeke baada ya kufunga bao la nane na kuamsha nderemo na vifijo kwa maelfu ya mashabiki wao waliohudhura uwanjani hapa.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Temeke Daudi Siang’a  alisema kuwa walistahili kushinda kutokana na kuwaandaa vijana wake kikamilifu kwa ajili ya mashindano haya, hivyo haoni kama kuna timu ya kuwazuia msimu huu.
“Timu yangu ilicheza vizuri na ilistahili ushindi kwa sababu kisaikolojia wachezajji wangu wako vizuri, lakini vile vile niliwapa muda mrefu wa maandalizi yenye mbinu madhubuti, kwa ushindi wa leo kwetu si wa kubahatisha”, alisema Siang’a.
Kwa upande wake, kocha wa Arusha Gefrey Mrope alisema kuwa, hofu ya mashindano juu ya vijana wake ndio sababu kubwa ya kupoteza mchezo wa leo kwa kuungwa idadi kubwa ya mabao lakini aliaahidi kufanya marekebishao katika hilo.
“Kisaikolojia wachezaji wangu wengi ni wapya hivyo hawana uzoefu wa kucheza katika kadamnasi kubwa ya watu kama hii, lakini naahidi kulifanyia kazi jambo hilo ili katika mchezo ujao, tuweze kupata ushindi”, alisema Mrope

No comments: