Abbott alikuwa amekabiliwa na wakati mgumu uongozini
Australia
inaelekea kupata waziri mkuu mpya baada ya Tony Abbott kuondolewa
uongozini katika chama cha Liberal na waziri mmoja wa chama chake.
Kwenye
uchaguzi wa kiongozi wa chama uliofanywa haraka, Bw Abbott, ambaye
umaarufu wake umekuwa ukididimia kwa mujibu wa kura za maoni, alipata
kura 44 huku waziri wake Bw Malcolm Turnbull akipata kura 54.
Wabunge wa chama hicho hata hivyo walimpigia kura Julie Bishop kusalia kama naibu kiongozi wa chama hicho.
Bw Turnbull anatarajiwa kuapishwa baada ya Bw Abbott kumwandikia gavana mkuu na kujiuzulu.
Mapema
Jumatatu, kwenye kikao na wanahabari Canberra, Bw Turnbull alisema iwapo
Bw Abbott angesalia kiongozi wa chama hicho, serikali ya muungano
ingeshindwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Alisema
ilikuwa vigumu kwake kufanya uamuzi huo, lakini kwamba ni “wazi kuwa
serikali haijafanikiwa katika kutoa uongozi wa kiuchumi unaohitajika” na
kwamba Australia inahitaji mtindo mpya wa uongozi.
Bw Turnbull atakuwa waziri mkuu wa nne wa Australia tangu 2013.
Waziri
mkuu wa chama cha Leba Julia Gillard aliondolewa uongozini na Kevin Rudd
kwenye kura ya uongozi wa chama Juni 2013, miezi kadha kabla ya
uchaguzi mkuu ambao chama cha Liberal, chake Tony Abbott, kilishinda.
Bi Gillard mwenyewe alikuwa amemuondoa Rudd kama waziri mkuu 2010.
No comments:
Post a Comment