SHABIB: CCM GAIRO MBELE KWA MBELE - LEKULE

Breaking

8 Sept 2015

SHABIB: CCM GAIRO MBELE KWA MBELE



ShabbbMgombea Ubunge wa jimbo la Gairo kwa tiketi ya CCM, Ahmed Shabiby.
Nimeamua kugombea tena ubunge kwa sababu najua wananchi wa Gairo wananihitaji, mafanikio makubwa niliyowaletea katika kipindi chote nilichokuwa mbunge yamewafurahisha na wanaamini kwamba mimi ndiye mkombozi wao.

“Kwa kipindi chote nilichokuwa madarakani nimeshafanya mambo mengi ya kuwasaidia wananchi na wao ni mashahidi wa hilo ndiyo maana wananihitaji nigombee tena.
“Nimefanikisha upatikanaji wa maji Gairo, tatizo ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa likiwasumbua wananchi wangu. Nimewezesha wakulima kupata matrekta ambayo wanayatumia kwa shughuli zao za kilimo na Kituo cha Afya cha Gairo sasa kina chumba cha upasuaji.
“Barabara zinapitika majira yote na kiwango cha elimu kimepanda tofauti na kabla sijaingia madarakani, Gairo ya sasa siyo ile niliyoikuta wakati naingia madarakani na wananchi wangu ni mashahidi wa hilo,” anasema mbunge wa Gairo anayemaliza muda wake, Mheshimiwa Ahmed Shabib ambaye ameamua kugombea tena kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mahojiano maalum na Uwazi, Shabib ambaye mbali na siasa pia ni mjasiriamali mkubwa anayemiliki vitega uchumi vingi, akitoa ajira kwa vijana wengi wa Gairo na sehemu nyingine Tanzania, anasema ameamua kugombea tena ubunge kutokana na kiu yake ya kuwaletea wananchi wa Gairo mafanikio.

KWA NINI ANAGOMBEA TENA?
“Nataka kuwaletea maendeleo makubwa zaidi wananchi wa Gairo, nimeshafanya mambo makubwa ya kimaendeleo lakini naona bado haitoshi, nahitaji muda zaidi wa kuendelea kuwasaidia wananchi wangu, ndani ya kipindi kifupi nilichokaa madarakani, tayari nimetatua kero kubwa zilizokuwa zinawakabili wananchi wangu na bado nahitaji kuendelea kuwasaidia.
“Ushirikiano walionipa kwa kipindi chote nilichokuwa madarakani umesababisha hata yale matatizo ya wananchi ambayo awali yalikuwa yanaonekana kuwa kero kubwa yapatiwe ufumbuzi wa kudumu,” anasema Mheshimiwa Shabib.

VIPAUMBELE VYAKE NI VIPI?
“Nawaomba wananchi wa Gairo wanipe tena nafasi ya kuwaongoza kwa sababu kama kawaida yangu, mimi si mtu wa maneno mengi, nafanya kazi ambayo kila mtu anaiona. Nipo tofauti na wanasiasa wengi.
“Vipaumbele vyangu ni kuboresha huduma za afya kwa watu wote hasa kwa akina mama wajawazito, watoto na wazee. Tayari kituo chetu cha afya Gairo kinafanya upasuaji, madaktari na manesi wapo wa kutosha na malengo yangu ni kuhakikisha naboresha zaidi huduma za afya, sitaki kabisa kuona mtu anapoteza maisha kwa sababu amekosa dawa au huduma. Hilo nitalisimamia kwa vitendo.
“Kipaumbele kingine ni suala la elimu, nimejitahidi sana kwa kipindi chote nilichokuwa madarakani kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini, kuhakikisha kuna walimu wa kutosha na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
“Nimewezesha Shule ya Sekondari ya Gairo (G Sec) kuwa na kidato cha tano na sita, kuwa na walimu wa kutosha na vifaa muhimu. Malengo yangu ni kuhakikisha elimu ya Gairo inazidi kupanda chati na hilo litawezekana endapo wananchi wangu watanipa tena ridhaa ya kuwaongoza.
“Suala la maji kwa sasa siyo tatizo jimboni kwangu lakini naona kama haitoshi, nataka kuhakikisha wananchi wote mpaka wa vijijini kabisa wanapata maji safi na salama kwa muda wote. Miradi mikubwa ya kusambaza maji inaendelea kwenye vijiji vyote na wananchi wangu ni mashahidi wa hilo.
“Kwa upande wa kuwawezesha wananchi wangu, nataka kuwasaidia wanawake na vijana kupata mikopo na mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kimaisha. Naamini ukimuwezesha mwanamke basi umeikomboa jamii nzima, hali kadhalika ukimuwezesha kijana basi umewasaidia wengi ambao wapo nyuma yake.
“Nataka kuwaona wanawake na vijana wakifanya biashara ndani na nje ya Gairo, fursa zipo nyingi, kuanzia kwenye kilimo cha kibiashara, ufugaji na sehemu nyingine nyingi,” alisema Shabib.

ANAWAZUNGUMZIAJE WAPINZANI?
Kutokana na heshima ya uchapakazi na kuwajali wananchi kwa kuyashughulikia kikamilifu matatizo ya wananchi wangu, sina wasiwasi kabisa na wapinzani. Kwa kifupi Gairo ni kama hakuna upinzani kwa sababu hao wapinzani waliopo, hawazungumzii sera zao badala yake wana kazi ya kuhubiri matusi, chuki na uhasama kwa wananchi wangu. Watanzania hawataki siasa za namna hiyo, wanataka kusikia sera, kwa kuwa wao hawana sera wanachoweza ni kutukana majukwaani tu.
“Hata wakipambana vipi hawataweza kushinda kwa sababu wananchi wangu wanaelewa tofauti kati ya siasa chafu na siasa za kiungwana. Wanazungumza sana kuhusu mimi hasa kutokana na biashara zangu zikiwemo za mabasi ya abiria na hoteli. Hawajui kwamba nilikuwa nafanya biashara hata kabla sijawa mbunge.
“Hata kwa upande wa urais, hakuna chama cha upinzani kinachoweza kuingia ikulu isipokuwa CCM pekee, wananchi wawe makini kuchagua watu wenye sifa na vigezo vya kutawala nchi na John Pombe Magufuli ndiyo chaguo sahihi. CCM Gairo mbele kwa mbele! CCM Tanzania hakuna mpinzani.

No comments: