RAIS
wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere
aliwahi kuwaambia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa, wananchi
wanataka mabadiliko, akasema wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje
ya CCM.
Maneno haya ya Mwalimu ni nguzo ya CCM,
kwamba uhai wa chama hicho hautatokana tena na ukongwe wake bali mfumo
wa mabadiliko ambao rais wa kwanza aliuona kuwa ndiyo kiu ya wananchi
wengi hivi sasa.
Kiu
ya mabadiliko aliyoiona kiongozi huyo wa zamani wa CCM ilikwenda mbali
zaidi kiasi cha kuwafanya wananchi wawe tayari kukihama chama
kilichowalea kwa miaka nenda rudi na kujitafutia mabadiliko nje ya chama
hicho kikongwe.
Nilitaraji viongozi wa chama hicho hasa
katika kipindi hiki cha uchaguzi wangetambua maono ya Nyerere na
kuyaishi kwa lengo la kukinusuru chama kisianguke.
Pengine msemo wa wahenga una maana;
kwamba sikio la kufa halisikii dawa ndiyo maana CCM inapuuza wosia huo
wa mabadiliko na sasa kinajikita katika siasa za kushambulia watu kwa
kutumia mbinu mbalimbali.
Nashibisha hoja; akiwa kwenye moja ya
kampeni zake za urais mgombea wa vyama vinavyoundwa na Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa hivi karibuni mkoani Tabora
alipokelewa na mabango mbalimbali lakini moja lililokuwa na maana kwangu
lilisomeka hivi:
“Lowassa angekuwa shetani, Magufuli
(John, mgombea wa CCM) angekuwa Mungu tungemchagua shetani kwani
tumeichoka CCM.” Ni maneno machache lakini yana maana kubwa. Kwamba
wananchi wako tayari kumbadili Mungu kwa shetani.
Hoja ni ‘wananchi kutaka mabadiliko’
siyo kitu kingine. Siyo ushetani wa mgombea fulani wa chama fulani, watu
wako tayari kukata kiu yao ya mabadiliko mahali popote, amshaamsha ya
upinzani inachochewa na kiu ya mabadiliko, si kitu kingine.
Hoja za mgombea urais wa Ukawa kuwa
fisadi, mgonjwa, siyo msafi, amekumbatia mtandao wa wezi zinaeleweka
kama bango la wananchi wa Tabora lilivyosomeka kwamba wao wako tayari
kumchagua shetani ili tu wapate mabadiliko.
Katika hili CCM wanashindwa nini
kubadili gia angani, wanakwazwa na kipi mpaka wasiwapatie wananchi
mabadiliko wayatakayo? Kuna ugumu gani wa kuwaaminisha wananchi kuwa
chama kitakachokata kiu ya mabadiliko ni CCM?
Ahadi: CCM iko tayari kujisahihisha
yenyewe kwanza. Serikali yake italeta mabadiliko ya mfumo wa afya,
elimu, utumishi, utoaji haki, usimamizi wa rasilimali za nchi na
mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa serikali kwa ujumla wake kwa
lengo la kuwatoa wananchi kwenye hali ya umaskini. CCM ikijinadi hivi
haitashangiliwa kweli?
Naweza kuulizwa na CCM; tumekuomba
ushauri? Hakika nitasema la! Lakini uungwana ni vitendo. Naandika haya
kukisaidia mawazo chama hiki kikongwe kijitambue ili kijiweke kwenye
misingi mizuri ya kushindana katika uchaguzi huu na kupata ushindi wa
haki ambao utalinusuru taifa hili na vurugu.
Niwaambie wanaoendesha kampeni za
majukwaani wakitaka kushawishi umma hawana budi kurudi kwenye msingi wa
mabadiliko. Wamnadi mgombea wao kuwa ni mtu atakayeweza kuwasaidia
wananchi kupata wanachokihitaji, waache kumshambulia mtu ambaye wamekuwa
naye kwenye uongozi miaka nenda rudi akiwa msafi au mchafu.
Kwangu mimi huu si wakati wa CCM kumsema
Lowassa, ni wakati wa kueneza sera za mabadiliko yatakayolitoa taifa
hili kutoka hapa tulipo kwenda mahali pengine pazuri zaidi. Mambo ya
ufisadi tuviachie vyombo vya usalama vishughulike na watuhumiwa.
Kumsakama mtu majukwaani ni kumtafutia huruma kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment