Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
SERIKALI
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia
itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Takwimu Huria Kanda ya Afrika.
Mkutano
huo utakaofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete utafanyika tarehe 4 – 5 Septemba, 2015 katika
Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Kauli Mbiu ni “Tumia Takwimu Huria Kuendeleza Afrika” (Developing
Africa Through Open Data).
Washiriki
takribani 400 kutoka Serikalini, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi,
Taasisi za Elimu ya Juu na Washirika wa Maendeleo kutoka ndani na nje ya
Nchi wanatarajiwa kushiriki.
Miongoni
mwa washiriki kutoka Serikalini ni pamoja na Wakurugenzi kutoka Idara
za Sera na Mipango, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA na Maofisa Takwimu
Waandamizi wa Wizara zote.
Mkutano
wa Takwimu Huria kwa Kanda ya Afrika ni wa kwanza wa aina yake Barani
Afrika Tanzania ikiwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji.
Heshima
hiyo imetokana na Tanzania kujiunga na Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli
za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership – OGP) unaolenga
kuifanya Serikali kuwa wazi zaidi na hivyo kuleta uadilifu na
uwajibikaji katika kuwahudumia Wananchi.
Katika
utekelezaji wa Mpango wa OGP, Tanzania iliweka kipaumbele katika
kuanzisha Tovuti ya Takwimu Huria itakayoweka wazi takwimu mbalimbali za
Serikali na Taasisi zake.
Madhumuni ya Mkutano ni kujadiliana kuhusu mfumo wa Takwimu Huria na jinsi utakavyoleta maendeleo hususan kwa nchi za Afrika.
Mkutano
utawawezesha wadau kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu mfumo wa
Takwimu Huria na kuona jinsi gani Sera za nchi zenye mfumo huo
zinavyofanya kazi na kusimamia viwango vya upatikanaji wa Takwimu Huria.
Aidha,
Mkutano huo utaihusisha sekta binafsi na wadau wengine katika matumizi
ya Takwimu Huria katika kuleta maendeleo ya kasi zaidi Barani Afrika.
Washiriki
watajadili jinsi ya kukuza na kuimarisha matumizi ya Mfumo wa Takwimu
Huria katika kutoa huduma kwa wananchi hasa katika sekta ya Huduma za
Jamii za elimu, afya, maji na kilimo.
Tunaomba ushirikiano wenu ili Mkutano huu ufanyike na kukamilika kwa ufanisi.
Imetolewa na Ofisi ya Rais, Ikulu
No comments:
Post a Comment