Wakati
tafiti za kienyeji zenye lengo la kupima kukubalika kwa wagombea urais,
hasa Dk John Magufuli na Edward Lowassa zikizidi kuongezeka, polisi
jijini Arusha mwishoni mwa wiki walitumia nguvu kutawanya vijana
waliokuwa wakiendesha kura za maoni kwenye stendi ndogo ya mabasi na
soko kuu.
Tangu
kutangazwa kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi za Twaweza na
Ipsos, vijana kwenye maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko, hasa sokoni na
kwenye baa wamekuwa wakiendesha tafiti zao za kienyeji wakiwa na lengo
la kuonyesha hali halisi ilivyo mitaani tofauti na matokeo ya tafiti
hizo mbili.
Katika
tafiti hizo za Ipsos na Twaweza, Dk Magufuli, ambaye anagombea urais
kwa tiketi ya CCM, alikuwa mbele ya Lowassa anayegombea kwa tiketi ya
Chadema na vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
lakini matokeo hayo yamepingwa vikali na wadau mbalimbali, huku
yakiamsha tafiti za kienyeji mitaani.
Katika
tukio lililotokea mjini Arusha, vijana walikuwa wakiendesha utafiti wao
kwenye soko kuu la Arusha na eneo la kituo kidogo cha mabasi, lakini
polisi walifika na kuwatimua wakidai wanavunja sheria.
Wafanyabiashara
hao wa soko hilo na stendi ndogo, waliandaa maboksi mawili ya kura,
moja likiwa limeandikwa “Magufuli” na jingine “Lowassa”. Baadaye
walialika watu kwenda kupiga kura.
Kila
aliyepita katika eneo hilo alielezwa utaratibu wa kupiga kura na
alitumbukiza karatasi yake katika boksi lililoandikwa jina la mgombea
anayeona anafaa kuwa rais.
Utafiti wa stendi ndogo ulikamilika baada ya muda na ulionyesha matokeo ya wagombea hao (tunayo).
Wakati
watu waliokuwa stendi ndogo wakiendelea kushangilia matokeo hayo,
wafanyabiashara wenzao wa soko kuu walikuwa wakiendelea kupiga kura na
ghafla polisi walifika maeneo hayo na kuwatimua vijana waliokuwa
wakikusanya kura.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema waliokuwa
wanafanya utafiti huo walikiuka sheria na kwamba kitendo chao kingeweza
kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa kulikuwa na watu wasioafikiana.
Aliwataka wakazi wa Arusha kuacha kufanya mambo ambayo hayana manufaa, badala yake wasubiri siku ya kupiga kura.
“Huo ni utafiti wa aina gani wa maboksi?” alihoji alipoulizwa kuhusu tukio hilo.
“Hizi ni vurugu za mitaani. Tunawaomba wananchi watulie, wasubiri siku ya uchaguzi wapige kura kwa amani.”
Hili
ni tukio la pili la utafiti unaofanywa kienyeji mitaani baada ya
wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam kuendesha utafiti wao kwa
kuruhusu watu kumpigia kura mgombea wanayempenda kati ya Magufuli na
Lowassa.
Mbali
na utafiti huo wa wakazi wa Dar es Salaam, kwenye maeneo mengine nchini
kumekuwapo na watu wanaoendesha tafiti kama hizo zenye lengo la kujua
ni mgombea gani wa urais anakubalika zaidi.