Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Peter Elias ameondolewa kwenye kikosi cha waandishi wa habari wanaoandika habari za kampeni za uchaguzi za mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kwa madai kuwa aliandika habari isiyostahili.
Hii
ni mara ya pili kwa CCM kumtimua mwandishi wa gazeti hilo kutoka kwenye
msafara wa mgombea wake wa urais. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2010
wakati ilipomtimua Midraj Ibrahim kwa kuripoti tukio ambalo chama hicho
kikongwe hakikupenda litangazwe kwenye vyombo vya habari.
CCM
imesema imechukizwa na kitendo cha mwandishi huyo kuripoti habari ya
tukio la wanachama wa Chadema kumnyooshea alama ya vidole viwili na kumzomea mgombea wa CCM wakati aliposimama Uyole, Mbeya. Alama ya vidole viwili ni nembo iliyo kwenye bendera ya Chadema.
Elias
amesema kuwa juzi mkurugenzi wa mawasiliano wa CCM, Godfrey Chongolo
ndiye aliyemweleza kwamba chama hicho kimesikitishwa na habari hiyo,
akidai kuwa kulikuwa na habari nyingi zaidi zinazomhusu mgombea huyo wa
urais.
Elias
alisema alielezwa na Chongolo kuwa CCM imeshindwa kuvumilia habari ya
magufuli kuzomewa akisema haikustahili kupewa uzito.
Mkurugenzi huyo alimwambia mwandishi huyo kuwa alitarajia kuona taarifa hiyo ikiripotiwa “Vijana wa Chadema wafanya fujo kwenye mkutano wa kampeni wa Dk Magufuli.”
Kutokana
na habari hiyo, Chongolo alimtaka Elias kutoendelea kubaki katika
kikosi cha waandishi kwa sababu anawaharibia katika vita wanayopigana
kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
“Unajua
sisi tuko vitani, kwa hiyo unapoandika kwamba Wanachadema walimzomea
kwa kuonyesha vidole viwili juu, maana yake ni kwamba hawamkubali
mgombea wetu, sasa hapo unawaeleza nini Watanzania?”
“Siku
ile ya tukio Magufuli alifanya mikutano ya barabarani zaidi ya mitano,
nashangaa ninyi mkaona ile ndiyo habari ya kuandika na kuacha nyingine
za maana,” alisema Elias akimnukuu Chongolo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema amesikia na baadaye akakata simu.
Akizungumzia
uamuzi huo Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu amesema kampuni
imesikitishwa na hatua hiyo lakini haitakatishwa tamaa katika
kutekeleza majukumu yake kwa umma.