MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema kura zote za urais, ubunge na udiwani, zitahesabiwa katika vituo vya kupigia kura na matokeo yote kutangazwa hapo hapo na ni marufuku kusafirisha masanduku ya kura kama ilivyokuwa zamani.
Jaji Lubuva aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano na
wawakilishi wa walemavu kujadili namna bora ya wao kushiriki katika
Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu ni marufuku kuhamisha masanduku
ya kura kwa sababu vituo vya kupigia kura vitabadilika kuwa vituo vya
kuhesabia kura baada ya upigaji kura kumalizika.
“Kura zote za urais, ubunge na udiwani zitahesabiwa katika kila kituo
na matokeo yatabandikwa vituoni hapo hivyo sijui wanaosema kura
zitaibiwa zitaibiwaje,” alisema JajiLubuva na kuongeza:
“Baada ya matokeo kubandikwa katika kila kituo yatapelekwa katika kata husika kujumlishwa na hapo pia yatabandikwa.
“Mshindi wa udiwani atatangazwa hapo na yale ya ubunge na urais
yatapelekwa jimboni ambako yatajumlishwa na mshindi wa ubunge
atatangazwa na kukabidhiwa cheti huku ya urais yakipelekwa makao makuu
ya Tume.
“Matokeo ya urais yatabandikwa katika kila jimbo na fomu ile ya
matokeo itaskaniwa na kutumwa moja kwa moja makao makuu ya tume kwa
kupitia mkongo wa mawasiliano wa taifa badala ya simu za mkononi kama
ilivyokuwa awali,” alisema Lubuva.
Alisema njia hiyo itasaidia matokeo kufika kwa haraka kama
inavyotakiwa na baada ya tume kupokea matokeo hayo itakuwa ikiyatangaza
moja kwa moja kupitia luninga na redio.
Jaji Lubuva alisema njia nyingine iliyoandaliwa ya kutuma matokeo ni
kwa nukushi (fax) ambako halmashauri zote nchini zimepatiwa vifaa
vitakavyoziwezesha kuyatuma matokeo haraka.
Alisema hatua ya tume kutangaza matokeo hayo kupitia luninga na redio
itasaidia wananchi kulinganisha matokeo watakayokuwa nayo na
yatakayokuwa yanatangazwa na tume.
Kutokana na hali hiyo alivishauri vyama vya siasa viache kauli za
kuwataka wafuasi wao wasiondoke vituoni baada ya kupiga kura kwa vile
hakuna kura zitakazoibiwa.
“Sioni haja ya vyama kusema vinalinda kura kwa sababu kura zote
zinabaki vituoni na zitahesabiwa palepale tofauti na zamani ambako
zilikuwa zikipelekwa kata na jimboni kuhesabiwa,” alisema.
Jaji Lubuva pia alivitaka vyama vya siasa kuacha kuingilia majukumu
ya Tume hiyo ikiwamo kuhoji mabadiliko ya watendaji yanayofanywa ndani
ya taasisi hiyo.
“Navishauri vyama vya siasa viache kuingilia majukumu ya Tume,
haviwezi kutuchagulia na kutuambia pale weka karani fulani hapa fanya
hivi… waache kuingia jikoni wasubiri chakula kipikwe watakula kwa haki
wala wasiogope,” alisema.
Ametoa kauli hiyo siku chache baada ya vyombo vya habari kumnukuu
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akisema
Mkurugenzi wa Tehama wa Tume hiyo, Sisti Cariah ameondolewa katika
nafasi hiyo huku akihusisha mabadiliko hayo na maandalizi ya kuiba
kura.
Hata hivyo NEC ilikanusha taarifa hizo ikisema hakuna mtu yeyote
aliyehamishwa katika idara zake zote isipokuwa wakuu hao wa idara
walichelewa kuwasilisha picha zao ndiyo sababu hawajaingizwa katika
orodha iliyomo katika tovuti ya Tume.
Jaji Lubuva alisema daftari la mwisho la wapiga kura litakamilika
baada ya wiki mbili hadi tatu na wapiga kura watapata fursa ya
kulihakiki kwa siku nane kabla ya uchaguzi.