MKURUGENZI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima amedai kushangazwa na taarifa za kuondolewa kwa baadhi ya watumishi wa tume hiyo na kuingizwa wapya wanaotajwa kuwa Usalama wa Taifa (TISS).
Amesema,
vyombo vya usalama vimeimarisha ulinzi kwenye Ofisi za NEC lakini
hakuna ukweli wa taarifa kwamba, Usalama wa Taifa ‘wameajiriwa kwa kazi
maalumu’ kama inavyoelezwa.
“Ni
kweli ofisi zetu za tume zinalindwa zaidi kwa sasa na vyombo vya
usalama kuanzia Makao Makuu yetu mpaka wilayani ili vifaa vya uchaguzi
viwe salama na sio vinginevyo kama inavyopotoshwa kuwa Maofisa Usalama
wa Taifa wamejaa,” anasema.
Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, Freeman Mbowe wakati akihutubia mkutano wa hadhara juzi kwenye Jimbo la Vunjo, Kilimanjaro alisema, “NEC haipo salama tena kwani imeingiliwa na watu wa Usalama wa Taifa kwa sasa.”
“viongozi
wengi wa Tume ya Taifa Uchaguzi kwa sasa wanaondolewa na nafasi zao
kuchukuliwa na watu wa Usalama wa Taifa ili kuweza kufanikisha malengo
ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kushinda kwa hujuma katika uchaguzi
huu,” Mbowe amenukuliwa.
Akizungumza
moja kwa moja kupitia Kituo cha Redio cha Magic FM jana asubuhi,
mkurugenzi huyo alisema, kauli zinazotolewa na Mbowe si za kweli.
“Sheria
za nchi huwa hazisimami kupisha uchaguzi mkuu, rais anayo mamlaka ya
kisheria ya kuteua kiongozi yoyote kwa mujibu wa mamlaka yake na sheria
za utumishi wa Umma zinaruhusu mtu kuhamishwa eneo la kazi. Shida iko
wapi?” alihoji Kailima.
Kuhusu
uteuzi huo kufanywa kwa lengo la kisiasa na kutengeneza mazingira ya
ushindi kwa CCM, Kailima alikana kuwepo kwa uhalisia wa taarifa hizo.
“Wanaofuatilia
masuala ya kisiasa watakubaliana na mimi hata mwaka 2000, 2005 na 2010
watumishi wa tume walikuwa wakibadilishwa karibu na kipindi cha
uchaguzi, sasa sijui huu uzushi unaosemwa una lengo gani?” Alihoji.
Hofu
imetanda miongoni mwa vyama vya upinzani kutokana na panga pangua ya
watumishi wa NEC inayofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika kipindi hiki
cha karibia uchaguzi.