Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Moshi Mjini, Zakaria Laizer amepewa likizo ya lazima ya siku 30, akituhumiwa kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Kiini
cha kupewa likizo hiyo kinatokana na kukutwa akipata chakula na
viongozi wawili wa zamani wa CCM katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha,
ambao sasa wamehamia Chadema.
Viongozi
hao ni katibu wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa mkoa wa Arusha, Issack
Kapriano maarufu Kadogoo na Katibu wa zamani wa Uchumi na Fedha mkoa
Kilimanjaro, Paul Matemu.
Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi, Loti Ole Nesele ametithibitishia jana kuwa Laizer kapewa likizo hadi baada ya uchaguzi.
“Miye
sipo Moshi niko Babati, lakini ni kweli alipewa barua hiyo ya likizo
wiki iliyopita, ukiniuliza sababu sitakwambia kwa sababu ni siri za
mtumishi na ofisi,” alisema.
Hata
hivyo, chanzo cha habari cha uhakika kinasema, Kadogoo ambaye ana
undugu na Laizer alimpigia simu ndugu yake huyo akimjulisha kuwa
angepita Moshi akienda Mwanga, hivyo amsaidie kumwekea oda ya chakula,
naye akafanya hivyo katika mgahawa wa East African ambapo walikutwa na
kiongozi mmoja wa CCM.
Mtu
aliye karibu na Kadogoo, alisema katibu huyo alimpigia simu Matemu
ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi ili ajumuike nao chakula cha jioni.
Taarifa
hizo zinadai siku iliyofuata, Laizer aliitwa na kuhojiwa na viongozi wa
CCM, lakini akajitetea kuwa Kadogoo ni mjomba wake na asingeweza
kumtenga kwa vile amehamia Chadema.
Laizer ni miongoni mwa wana- CCM waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.
Kutokana
na tuhuma za kuendelea kushirikiana na mgombea huyo wa Ukawa, viongozi
hao walipendekeza kwa uongozi wa mkoa wa Jumuiya hiyo umpe likizo ya
lazima Laizer kwa siku 30, ili arejee baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika.
Laizer
alipoulizwa kuhusu likizo hiyo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo
lakini mwenzake, Matemu licha ya kukiri kukaa meza moja na Laizer siku
hiyo, alieleza kushangazwa na likizo akisema mjumuiko walioufanya
haukuwa na ajenda yoyote ya kisiasa.
“Nimejiuliza
maswali mengi lakini sipati majibu. Kwamba CCM imefika mahali inataka
wana CCM wasichanganyikane na wafuasi wa vyama vingine. CCM wanataka
kufanya siasa ni uadui?” alihoji.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM mkoa Kilimanjaro, Festo Kilawe, alipoulizwa
kuhusu sakata hilo, aliomba aulizwe katibu wa jumuiya hiyo mkoa wa
Kilimanjaro, Robert Chilamato.
Hata hivyo, Chilamato ambaye ndiye aliyesaini barua ya likizo hiyo, alitaka watafutwe viongozi wa wilaya wa jumuiya hiyo. “Hilo jambo waulizwe viongozi wa wilaya (wa jumuiya) kwa vile mimi ni kiongozi wa ngazi ya mkoa,” alidai Chilamato.