Melela Kololo Hawaioni Ajenda Yao Kuu Kwenye Mijadala Ya Uchaguzi! - LEKULE

Breaking

23 Sept 2015

Melela Kololo Hawaioni Ajenda Yao Kuu Kwenye Mijadala Ya Uchaguzi!


Ndugu zangu,
Nimebahatika kutembelea maeneo mengi ya vijijini. Nahofia, kuwa wakati mwingine ninachokiona na kukitafsiri kwa maandiko kuna ambao hawakioni.
Napenda sana kudadisi ili kujifunza. Vijijini ninakokwenda najitahidi kuwadadisi na kisha kuwasikiliza watu wazima kwa vijana.
Niliyoyaona na kuyasikia pale Melela Kololo leo asubuhi, nimeyasikia kwetu Mbarali, Mpwapwa, Kondoa na kwingineko nilikobahatika kufika.
Kwa vile najua , kama ilivyo katika sehemu nyingi za nchi kwa sasa, Wilaya ya Mvomero ina tatizo kubwa la migogoro ya wakulima na wafugaji, kwa niliokutana nao niliwadadisi kwa kuuliza maswali matatu;
Mosi; Je, unadhani ongezeko la mifugo hapa Melela Kololo linachangia mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji?
Pili; Je, unadhani ongezeko la watu hapa Melela Kololo linachangia mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji?
Kwa maswali hayo juu, kama jibu ni ndio au hapana, nilihitaji maelezo ya kwanini niliyemuuliza alijibu hivyo.
Tatu; Je, kuna sababu nyingine , mbali ya hizo zenye kupelekea uwepo wa migogoro ya ardhi kati ya Wakulima na Wafugaji?
Ndugu zangu,
Ni kwenye swali hilo la tatu ndipo wanakijiji hufunguka. Sababu nyingine ni nyingi, lakini, moja ya kwanza inayotajwa karibu na kila unayemwuliza swali hilo ni RUSHWA!
Migogoro ya ardhi inachangiwa sana na rushwa yenye kuwahusisha pia baadhi ya watendaji.
Wananchi wanafunguka kwa kusema wazi kuwa rushwa ya madaraka imepelekea baadhi ya watendaji hata wa ngazi za juu kujikwapulia na kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi. Maeneo hayo yamezungushiwa wigo na hayalimwi kwa miaka mingi sasa. Wafugaji wanakosa maeneo ya malisho na kusongamana na wakulima. Wanaamini, kuwa kama wahusika watachukuliwa hatua amani itarudi.
Mwingine ananiambia;
" Ona kule bonde la Mgongola, Mvomero, kiangazi wakulima wanalima bustani zao za mboga na wafugaji wanapitisha mifugo yao ipate maji. Wafugaji hawana pengine pa kwenda na wakulima wanategemea bonde hilo nyakati za kiangazi. Lazima ugomvi utatokea"
Hivyo, wananchi wengi ninaokutana na kuongea nao, iwe Melela Kololo au Mbarali Mbeya, kwao ajenda kuu ni udhibiti wa rasilimali ardhi ili iwanufaishe walio wengi; wakulima na wafugaji wa nchi hii. Na katika kudhibiti hilo, wangependa viongozi wenye kutaka kuchaguliwa, waeleze kwa ufasaha namna watakavyopambana na rushwa. Vile vile waainishe mikakati ya kuwachukulia hatua wawekezaji na hata baadhi ya viongozi na watendaji waliojinyakulia, bila kufuata taratibu, ikiwamo kuthibitishishwa na mikutano ya vijiji, maeneo makubwa ya ardhi ambayo hawayatumii kwa kilimo bali wameyahodhi tu.
Ndugu zangu,
Hayo ni baadhi tu.