MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli, amesema mafisadi hawawezi kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa wanamwogopa.
Dkt.
Magufuli aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara,uliofanyika
katika Viwanja vya Mvumi Misheni, Jimbo la Mtera,mkoani Dodoma.
"Mafisadi
hawawezi kunichagua kwa sababu wananiogopa ila wapo Watanzania wengi
wanaonipenda na kunikubali wakiwemo maskini wenzangu, wanyonge ambao
watanipa kura nyingi ili niweze kuwatumikia na kutetea masilahi yao," alisema.
Alimpongeza
mwanasiasa mkongwe, Mzee John Malecela kwa ujasiri wake wa kuendelea
kubaki CCM licha ya kushindwa katika mbio za kuwania nafasi ya urais
miaka iliyopita.
"Mzee
Malecela aliwahi kugombea uteuzi wa nafasi ya urais, lakini
hakufanikiwa na hakufikiria wala kuthubutu kuhama chama hata siku moja,
bado yupo na amekuwa msaada mkubwa," alisema.
Alisema
mbali ya kuukosa urais, pia aliangushwa kwenye nafasi ya ubunge wa
Jimbo la Mtera na Livingstone Lusinde lakini hakuhama chama. Alisema
anawashangaa waliohama CCM baada ya kukosa nafasi.
Aliwaomba
Watanzania wamchague aweze kubadilisha maisha yao na kukuza uchumi
akiwataka wasikubali kudanganywa na wapinzani ambao hawana sera wala
uzoefu wa kuongoza Serikali.
Akizungumzia
sera ya elimu bure, alisema hakuna sababu ya kukosa madawati wakati
nchi ina rasilimali kubwa ya miti; hivyo alitoa wito kwa Wakurugenzi
kukaa mkao wa kufanya kazi.
Livingstone Lusinde
Naye
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni za CCM na mgombea ubunge Jimbo la Mtera,
Lusinde alisema CHADEMA kimepoteza mwelekeo baada ya kuwapokea wanasiasa
waliowatuhumu kwa kashfa mbalimbali ndani na nje ya Bunge.