Zanzibar. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa siku 100 za uongozi wake,
atahakikisha anaingia mikataba na kampuni za mafuta na gesi asilia ili
zianze uchimbaji katika ardhi ya Zanzibar.
Maalim Seif
alisema hayo juzi kwenye viwanja vya Tibirinzi mkoani Kusini Pemba
alipokuwa akizungumza na wananchi na wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa.
Aliwaomba
wananchi wa Unguja na Pemba wampe ridhaa ya kuongoza visiwa vya
Zanzibar ili aweze kuwaletea maendeleo na kuahidi kufanya mabadiliko
hayo kwenye sekta ya mafuta na gesi ndani ya siku 100.
Alisema
kazi ya uongozi ni kuchapa kazi na kuwa na dhamira ya kweli ya kuleta
mabadiliko ya kiuchumi na kuweka misingi ya utawala bora, haki na
demokrasia.
Alisema kitu hicho kinawezekana na
kikiwezekana, wananchi watakuwa na moyo wa kujitolea katika kufanya kazi
za kuendeleza nchi yao.
“Mimi naamini hakuna
linaloshindikana kwa uwezo wa mwenyezi Mungu. Tabia ya wananchi wa
visiwani wanakuwa na uchungu na wivu na nchi yao, naamini hakuna
Mzanzibari asiyeipenda nchi yake, naamini na hiyo ndio tabia ya wananchi
wa visiwani ambao wanakuwa na wivu kama mume kwa mkewe,” alisema Maalim
huku akishangiliwa kwa kutaja wivu wa mume na mke.
Maalim
Seif alisema CCM wamewasaliti Wazanzibari kwa kushindwa kuwatetea ndani
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa mchakato wa kuunda Katiba
mpya.
Alisema walipokwenda Dodoma walisahau kero na shida za Wazanzibari walizozipata kwa muda wa miaka 50.
“CCM
kwa kweli walitusaliti Wazanzibari kwa sababu wamekwenda kutengeneza
Katiba Mpya lakini kufika kule wameufyata kabisaaaa! Sawa sawa…badala ya
kuwatetea Wazanzibari wamekwenda kusahau yote na wakaungana na wale
watu wasioitakia mema Zanzibar wakaupitisha mfumo wa serikali mbili
ambao ni mbaya,” alisema Seif, ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mkuu huyo wa zamani wa
Idara ya Uchumi na Mipango ya CCM alisema akipewa nafasi ya kuwa Rais,
ataweka misingi ya utawala bora, atapambana na rushwa kwa kuwadhibiti na
kuwashughulikia wala rushwa, kuinua uchumi kwa kushughulikia suala la
bandari huru ili kuinua wafanyabiashara wafanye biashara zao kwa uhuru
na urahisi zaidi kuliko walivyo sasa.
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Mansoor Yussuf Himid, ambaye alikuwa mwakilishi wa
Jimbo la Kiembe Samaki (CCM) na ambaye hivi sasa ni mshauri wa Maalim
Seif, alisema Wazanzibari wana hamu ya kupata kiongozi ambaye atajali
utu, haki na usawa huku akizingatia umoja, upendo na mshikamano.
“Tunamtaka
kiongozi ambaye anajua na kuheshimu utu wa mtu atakayewaunganisha
Wazanzibari wote bila ya kujali dini, kabila wala rangi ambaye jambo la
kuwaunganisha watu ni lazima kwake,” alisema.
“Na mimi
naamini ndani ya nafsi yangu kwamba mtu huyo si mwingine zaidi ya Maalim
Seif kwa hivyo namuombea kura zenu mumpe ridhaa ili atuongoze katika
usawa.”
Alisema Zanzibar pamoja na utajiri wake hakuna
ajira zaidi ya zile za mahoteli tu na za vikosi vya SMZ ambazo hutolewa
kila inapokaribia uchaguzi, halafu ukimalizika uchaguzi vijana hao
hutupwa.
“Ajira tulizo nazo ni mahotelini tu, sasa vijana wangapi watafanya kazi hotelini? Kwani tuna hoteli ngapi?” alihoji Mansoor.
No comments:
Post a Comment