Moshi. Polisi waliosimamia mtihani wa taifa wa kumaliza
darasa la saba katika baadhi ya wilaya za mkoa Kilimanjaro wamekuja juu
wakipinga kulipwa posho ya Sh22,500 kwa siku badala ya Sh40,000.
Wakati
polisi waliosimamia mtihani huo katika mikoa mingine nchini wakilipwa
posho ya Sh120,000 kwa siku tatu, polisi waliosimamia mitihani hiyo
mkoani Kilimanjaro walilipwa Sh67,500 tu.
“Kiwango
kipya cha posho kwa polisi kilichopitishwa mwaka huu ni Sh65,000 kwa
siku tukasema hata kama wameshindwa kulipa kiwango hicho wangetulipa
basi 40,000 kama wenzetu,” alidai mmoja wa polisi hao.
Polisi
katika wilaya ya Hai, wao wameenda mbali na kususia malipo hayo na hadi
jana mchana kulikuwa hakuna polisi aliyepokea malipo hayo ingawa
walisimamia vyema mitihani hiyo.
Halmashauri pekee
zinazodaiwa kulipa posho ya Sh40,000 kwa siku kama halmashauri nyingine
nchini ni Same na Mwanga huku halmashauri nyingine zikidaiwa kulipa
posho ya Sh22,500 kwa siku.
Kamanda wa Polisi mkoa
Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema posho hizo zimelipwa kulingana na
maelekezo ya Wizara na kwamba viwango vya posho viko tofauti kulingana
na majukumu wanayokabidhiwa. “Wale waliosimamia vituo teule ambavyo
ndivyo vinahifadhi mitihani na wale wanaosindikiza mitihani wao
wanalipwa posho ya Sh40,00 kwa siku na wale wanaosimamia tu ni sh22,500
kwa siku,” alisema.
No comments:
Post a Comment