Ajinyonga kwa katani baada ya kunyang’anywa mke - LEKULE

Breaking

12 Sept 2015

Ajinyonga kwa katani baada ya kunyang’anywa mke


Serengeti:
Mkazi wa kitongoji cha Mihuru, kijiji cha Kitarungu wilayani Serengeti, Mara amejinyonga kwa kutumia kamba ya katani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kukosa ng’ombe wa kulipa mahari.
Chacha Bruna (25) alijinyonga kati ya Septemba 7 na 8 usiku baada ya kunyaang’anywa mke kwa kukosa mahari hiyo ya ng’ombe.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Yohana Gimano alisema Bruna alifikia uamzi huo baada ya kunyang’anywa mwanamke kwa kushindwa kulipa mahari.
“Yeye ni mkazi wa Tarime lakini hapa kijijini kuna ukoo wao, alipofika hapa alimtorosha binti mmoja (Rhobi Samweli) akakaa naye kwa muda wa siku nne. Septemba 7 ndugu zake walimfuata huyo binti ili atoe mahari, akaambiwa atoe ng’ombe tisa, yeye akasema anaye mmoja, wakamfukuza mpaka atoe mahari ndipo apewe mke, usiku akaamua kujiua,” alisema.
Alisema kuwa kabla ya kuchukua uamzi huo akiwa na kamba ya katani alimwambia mwanamke mmoja kwenye mji aliokuwa anaishi kuwa haoni faida ya kuishi na kuwa siku hiyo ndiyo mwisho wake. Hata hivyo, hawakufuatilia kwa kuwa hawakutegemea kama angechukua uamzi huo.
“Asubuhi walikuta ananing’inia kwenye mti pembeni ya barabara akiwa ameshakufa. Inaonekana alijinyonga usiku ule ule kwa kuwa wanadai hata chakula cha usiku hawakula naye, walijua yuko katika matembezi ya kawaida,” alibainisha.
Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Kitarungu, Emmanuel Matiko ambaye ni jirani yake alisema waliugundua mwili huo asubuhi baada ya wanafunzi waliokuwa wakienda shule kuukuta mwili wake ukining’inia.
“Suala la yeye kunyang’anywa mwanamke linajulikana na alionekana mwenye mawazo sana baada ya kushindwa kuelewana na ndugu wa mchumba wake. Huenda ilimuathiri kisaikolojia na kukosa msaada wa ushauri,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Philip Karangi hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo. Hata hivyo, Polisi wilayani hapa wamesema uchunguzi wa tukio hilo umebaini kuwa chanzo cha kifo ni kujinyonga .

No comments: