Watuhumiwa wa Stakishari wapanda kizimbani - LEKULE

Breaking

12 Sept 2015

Watuhumiwa wa Stakishari wapanda kizimbani


Dar es Salaam.
 Watu wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba ya mauaji katika Kituo cha Polisi cha Staki Shari kilichopo Wilaya ya Ilala.
Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono akishirikiana na Mrakibu wa Polisi, Jackson Chidunda aliwataja washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa kuwa ni Omari Abdula Makota (28), Rajabu Ally Ulatule (22), Ramadhani Hamis Ulatule (20) na Fadhil Shaban Lukwembe (23).
Akiwasomea hati ya mashtaka washtakiwa hao, Kombakono alidai kuwa Julai 12, 2015 katika kituo cha Polisi cha Staki Shari washtakiwa hao kwa pamoja walimuua askari polisi D. 6952 Sajenti Adamu.
Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao pia waliwaua askari namba E 3962 Koplo Gaudini, E1279 Koplo Peter na G 3010 PC Anthony.
Kadhalika alidai kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa hao waliwaua Salehe Semkoko, Erick Swai na Jackline Duma na kwamba washtakiwa hao walifanya makosa hayo ya mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hawakuruhusiwa kuzungumza chochote kwa sababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika na washtakiwa walipelekwa rumande kwa sababu mashtaka hayo hayana dhamana.
Kesi imeahirishwa hadi Septemba 24, 2015 kesi hiyo itakapotajwa kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekwisha kamilika ama la.

No comments: