Watu watano wamekufa na wengine 39 kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria la kampuni ya Metro kuacha njia na kupinduka katika eneo la Manga, mpakani mwa mikoa ya Tanga na Pwani, chanzo kikidaiwa dereva alikuwa akisinzia.
Waliokufa
katika ajali hiyo iliyotokea jana ni Joseph John (45) na Joseph Shayo
(41), wakazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro na Zakaria Kintupa, mkazi wa
Lutindi na mwanawe ambaye jina lake halikufahamika mara moja.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji, amethibitisha kutokea kwa
ajali hiyo na kwamba miili ya marehemu na majeruhi wa ajali hiyo
wamepelekwa katika Kituo cha Afya cha Mkata, wilaya ya Handeni, mkoani
Tanga.
Kwa
mujibu wa Kamanda Mwombeji, ajali hiyo ilitokea saa 5.00 asubuhi
wakati basi hilo likitokea Dar es Salaam kuelekea Rombo, mkoani
Kilimanjaro.
Alisema basi hilo lilipinduka baada ya dereva kushindwa kumudu kona kali na hivyo kuacha njia na kuingia kwenye korongo.
Hata
hivyo, baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri na basi hilo walidai ajali
hiyo ilitokea kutokana na dereva kuendesha huku akisinzia.
Kamanda
Mwombeji alisema dereva wa basi hilo ambaye jina lake halikufahamika
alitoroka baada ya ajali hiyo kutokea na kwamba polisi wanaendelea
kumsaka, huku mmiliki wa basi akihojiwa na kwamba uchunguzi wa ajali
hiyo ili kujua chanzo chake halisi unaendelea.
No comments:
Post a Comment