Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amefunguka na kuwaomba Watanzania kumpa kura ambazo ameziita bakora ili awacharaze viboko watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi nchini.
Lowassa
ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia umati katika
mkutano wa kampeni kwenye Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, mjini
Morogoro.
Alisema
ili kutekeleza azima yake, ni vizuri wananchi wakajitokeza kwa wingi
kama Oktoba 25, mwaka huu kama walivyojitokeza jana wapige kura ili
kumpa kazi ya kuwanyoosha mafisadi.
Akizungumza
huku akikatizwa kutokana na kushangiliwa na umati, Lowassa alisema
Serikali yake itahakikisha inawashughulikia wale wote watakaotumia
vibaya fedha au madaraka waliopewa kinyume cha sheria na taratibu.
Lowassa
alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu mwaka 2008, kama njia ya kuwajibika
baada ya kuibuka kwa sakata ya serikali kuipa zabuni kampuni ya kufua
umeme ya Richmond katika mazingira tata.
Sakata
hilo liliibuliwa na Kamati Teule iliyoongozwa na Mbunge wa kyela, Dk.
Harrison Mwakyembe, baada ya kuchunguza na kuwasilisha ripoti bungeni.
Hata
hivyo, baadhi ya mahasibu wake wa kisiasa wamekuwa wakimhusisha na
tuhuma hizo, lakini ameshazikanusha na kuwataka wenye ushahidi kwenda
mahakamani vinginevyo wafunge midomo.
Kadhalika,
Lowasa ameshasema kuwa maagizo ya kuipa kampuni hiyo zabuni ya kufua
Megawati 100 za umeme wa dharura yalitoka mamlaka za juu.
Mama lishe,Bodaboda
Katika
hatua nyingine, Lowassa alisema kuwa atakapochaguliwa, Serikali yake
itahakikisha inaanzisha benki maalum ya maendeleo kwa ajili ya
mamalishe, waendesha bodaboda pamoja na wafanyabiashara ndogo ndogo
maarufu kama machinga.
Lowassa
alisema kuwa ataanzisha beki hiyo kwa kuwa ni moja ya mikakati ya
kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo pamoja na kuwatengenezea
mazingira mazuri ya kufanya biashara bila kubughudhiwa na mgambo.
Kufufua Viwanda
Kuhusu
viwanda vilivyokufa katika Mkoa wa Morogoro baada ya kubinafishwa,
alisema kuwa baada ya kuchaguliwa atahakikisha, anafanya utafiti wa
kuviangalia upya viwanda hivyo kama vinaweza kufufuliwa na Serikali au
kujengwa upya kwa ajili ya kutoa ajira kwa wakazi wa mkoa huo.
Alisema
mkoa huo kwa miaka kadhaa iliyopita ulikuwa wa viwanda na wakazi wake
walipata maendeleo, hivyo ni lazima asimamie kurudishwa kwa uchumi wa
viwanda kwa lengo la kuwasaidia wakazi wake.
Kilimo cha Kisasa
Kuhusu
kilimo, Lowassa alisema kuwa wananchi wengi wa mkoa huo wanategemea
zaidi kilimo, hivyo katika utawala wake atahakikisha wanawekewa
mazingira ya kulima kilimo cha kisasa pamoja na kuwapunguzia kodi ambazo
zinaonekana sio rafiki kwao.
Elimu ya Bure
Kwa
upande wa elimu, Lowassa alisema kuwa atakapochaguliwa, elimu itakuwa
bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne na kwamba elimu
itakayotolewa itakuwa bora na si bora elimu kama ilivyo sasa.
Alisema kuwa hayo yote hayatafanikiwa ikiwa wananchi hao hawatajitokeza kumpigia kura Oktoba 25, mwaka huu.
Sumaye: Msiogope
Kwa
Upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, aliwataka wananchi
kutotishika na vitisho vinavyotolewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kuwa upinzani ukiingia Ikulu kutakuwa na machafuko.
Sumaye
aliahidi kuwa Serikali ya Ukawa ikiingia madarakani itahakikisha
inasimamia mambo mbalimbali waliyoyaainisha kwenye ilani yao tofauti na
serikali ya CCM ambayo alisema licha ya kuahidi maisha bora na kukusanya
kodi za wananchi, bado hali ya maisha imeendelea kuwa mbaya siku hadi
siku.
Awali,
mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro kupitia Chadema, Albanie Marcus,
aliomba wananchi wa Manispaa ya Morogoro kumchagua katika nafasi hiyo
ili ashirikiane na Lowassa kurudisha viwanda 14 vilivyobadilishwa
matumizi yake.
Alisema
kuwa katika uongozi wake atahakikisha viwanda ambavyo vimebadilishwa
matumizi yake vinafufuliwa na kuwa sehemu ya ajira kwa wananchi wa Mkoa
wa Morogoro.
Marcus
alisema kuwa katika mji wa Morogoro huduma mbalimbali za kijamii
zikiwamo za barabara na afya hususani kwa wanawake na watoto zimezorota
na kusababisha vifo visivyo vya lazima na kuahidi kuwa wananchi
wakimchagua, atahakikisha anazisimamia na zinaboreshwa.
No comments:
Post a Comment