Mchakato wa usikilizwaji wa kesi ya Sheria ya Makosa ya Uhalifu wa Kimtandao umeanza, huku Mahakama Kuu nchini ikiipa Serikali siku 14 kuwasilisha mahakamani hapo majibu yake ya utetezi kuhusiana na kesi hiyo.
Kesi
hiyo namba 32 ya mwaka 2015 ilifunguliwa wiki iliyopita na Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), kwa kushirikiana na mashirika
mengine ya haki za binadamu, kikiwemo Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC) kupitia kwa wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole.
Jana
kesi hiyo ilianza kutajwa mahakamani hapo, ikiwa ni hatua za awali za
mchakato wa kuanza usikilizwaji wake, huku mahakama ikiiamuru serikali
hadi kufikia Septemba 18, iwe imewasilisha majibu yake ya utetezi.
Amri
hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Jopo la majaji watatu
wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Profesa John Ruhangisa, baada ya Serikali
kupitia kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Richard Kilanga kuomba muda
wa siku 14 kuwasilisha majibu hayo.
Pia
Jaji Ruhangisa kwa niaba ya majaji wenzake, Lugano Mwandambo na
Winfrida Koroso, alitoa amri kwa upande wa mdai, kuwasilisha majibu ya
ziada ya utetezi wa Serikali, ndani ya siku saba, zitakazo anza siku
Serikali itakapokuwa imewasilisha majibu yake.
Upande wa mdai jana uliwakilishwa na Wakili Benedict Ishabakati, pamoja na Wakili Kambole mwenyewe ambaye pia ndiye mdai.
Jaji
Ruhangisa alisema kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Oktoba 22,
2015, mchana, kwa ajili ya kupanga namna ya kuendesha usikilizaji wa
kesi hiyo.
Katika
kesi hiyo mdai anapinga baadhi ya vifungu vya sheria hiyo akidai kuwa
vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na
kwamba utekelezaji wake utakiuka haki mbalimbali za binadamu.
No comments:
Post a Comment