Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB Mkwizu akifungua mkutano wa
kwanza wa mwaka wa Serikali Mtandao leo jijini Arusha.Zaidi ya wataalam
wa TEHAMA 500 kutoka Wizara, Idara, Wakala,Taasisi, Halmashauri wako
jijini Arusha kujadili mafanikio na changamoto za Serikali mtandao.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt.Jabiri Bakari akitoa ufafanuzi kuhusu Serikali
Mtandao kwa washiriki wa Mkutano wa kwanza wa Serikali Mtandao
unaofanyika katika ukumbi wa AICC jijini Arusha leo.
Mtaalam wa masuala ya Serikali
Mtandao kutoka nchini Singapore Bw.Tan Kim akiwasilisha mada kuhusu
Umuhimu wa Serikali mtandao kwa washiriki wa Mkutano wa kwanza wa
Serikali mtandao unaofanyika jijini Arusha leo
Wataalam wa Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano kutoka maeneo mbalimbali nchini wakifuatilia Masuala
mbalimbali wakati wa mkutano wa kwanza wa mwaka wa Serikali mtandao
unaofanyika jijini Dar es salaam.
Picha na Aron Msigwa.
………………………………………………………………..
Na. Aron Msigwa -MAELEZO .ARUSHA.
Serikali imewataka watalaam wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) walio katika utumishi wa umma kote nchini kufanya
kazi zao kwa kuzingatia maadili, weledi na ubunifu ili kuwawezesha
wananchi kupata huduma za serikali kwa njia ya mtandao katika maeneo
mbalimbali na kuondoa malalamiko yanayotokana na utoaji wa huduma
usiokidhi viwango.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Arusha na Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB Mkwizu wakati
akifungua Mkutano wa kwanza wa mwaka wa Serikali mtandao wa Maofisa
TEHAMA kutoka Wizara, Idara,Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Amesema Watumishi wa umma wasipotimiza wajibu wao
kikamilifu wanasababisha malalamiko kwa wananchi na kuifanya Serikali
kushindwa kufikia malengo iliyojiwekea.
“Ni muhimu wote mtamtambue kuwa utumishi wa umma imara
hujenga serikali na Taifa imara, utumishi wa kufanya kazi kwa mazoea na
kusukumwa hauna tija kwa taifa letu” Amesema.
Ameongeza kuwa ili kufikia malengo ya kuimarisha utawala
bora na kuongeza tija na ufanisi Serikali imekuwa ikisisitiza matumizi
ya TEHAMA ili kuimarisha mawasiliano ya haraka, yenye uhakika na salama
ndani ya taasisi mbalimbali za Serikali; kuanzia kwenye Wizara, Mikoa
hadi ngazi za Halmashauri pamoja na Balozi mbalimbali nje ya nchi.
Amefafanua kuwa katika kupanua wigo wa upatikanaji wa
taarifa muhimu na kuimarisha usalama wa Serikali na raia wake Serikali
imeendelea kujenga na kuongeza uwezo wa kupambana na majanga kwa kutumia
teknolojia.
Aidha, amesema Serikali kwa kutambua mchango wa TEHAMA
inaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zikiwemo za baadhi
ya mifumo kutokuongea, kutowasiliana na kutobadilishana taarifa kati
ya taasisi na taasisi pia rudufu ya mifumo ambapo kila taasisi inakuwa
na juhudi za kipekee katika kusimika na kutumia miundombinu ya TEHAMA
ambayo ingeweza kutumiwa na zaidi ya taasisi moja pamoja na changamoto
ya mifumo kuwa na viwango vya usimikaji tofauti.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao
( e Government Agency) Dkt. Jabiri Bakari awali akiwakaribisha Wataalam
wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano waliohudhuria Kongamano hilo
amesema kuwa katika kuimarisha uwazi na upatikanaji wa Takwimu huria,
Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya TEHAMA ili kuwawezesha
wananchi kupata huduma zinazotolewa na Wizara na Taasisi kwa njia ya
mtandao.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya vizuri katika
kufanikisha lengo kubwa la kufikisha huduma kwa wananchi na kuongeza
kuwa mpango wa Serikali uliopo sasa ni kuwa na mfumo mmoja
utakaowezesha taarifa zote za wananchi kuwa katika sehemu moja.
Akizungumza kuhusu mkutano huo Dkt.Jabiri amesema kuwa
washiriki zaidi ya 500 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali watapata
fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano katika kutekeleza
jitihada za Serikali Mtandao nchini pamoja na Kutafuta ufumbuzi wa
changamoto za serikali mtandao zilizopo nchini ili kuleta maendeleo ya
kiuchumi na kijamii.
Aidha, wataalam wa TEHAMA wa Tanzania waliohudhuria
kongamano hilo watapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalam wengine
wanaohusika na Serikali Mtandao kutoka nchi zinazofanya vizuri katika
eneo la Serikali mtandao zikiwemo India na Singapore.
Ameongeza kuwa katika mkutano huo mada mbalimbali
zitajadiliwa zikijikita katika usimamizi wa Serikali Mtandao nchini
Tanzania, Hali ya miundombinu ya Serikali mtandao na Utekelezaji wa
Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa uwazi.
Mada nyingine zitahusu uimarishaji wa uwazi na Mfumo wa
Takwimu huria nchini Tanzania na uimarishaji wa huduma za Serikali
kupitia simu za mkononi na mifumo inayotumika kutoa huduma kwa wananchi.
Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Bw.Agostin Mapunda
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha amesema kuwa Matumizi ya
TEHAMA katika shughuli za Serikali yamerahisisha utendaji wa kazi na
kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema sasa wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali
zikiwemo za upataji wa hati za ardhi kwa haraka zaidi kupitia mifumo ya
TEHAMA iliyoanzishwa na serikali.
Ameongeza kuwa ni vema mabadiliko hayo yakaendelezwa
kutokana na umuhimu wake katika kufanikisha utendaji wa Serikali,
kupunguza muda na kuokoa gharama!
“Tuko kwenye njia sahihi ya kuufanya utendaji wa Serikali
kupata mafanikio kupitia mtandao, hali hii tunaona imepunguza matumizi
na gharama kubwa waliyokuwa wanaipata wananchi kufuata huduma ambazo
sasa zimerahisishwa kupitia mtandao”
Amefafanua kuwa wananchi sasa wanaweza kulipia ankara zao
za umeme, maji na huduma nyingine kupitia simu zao za mkononi jambo
ambalo hapo awali halikuwepo
No comments:
Post a Comment