Jumuiya
ya Wazanzibari waishio Nchini Marekani (ZADIA), imepongezwa kwa
kusaidia gurudumu la maendeleo ya Elimu visiwani Zanzibar.
Pongezi
hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Zanzibar Bw. Suleiman
Yahya Ame wakati wa kupokea mchango wa vitabu vya Ufundi na Mafunzo ya
Amali uliotolewa na ZADIA kwa ajili ya shule za ufundi visiwani humo.
Akizungumza
kama mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika mjini Zanzibar, Bw. Ame
pia aliwashukuru Wanadiaspora hao kwa kuendeleza juhudi za kujenga
jamii iliyoelimika Zanzibar.
Aliendelea
kusema “Tukiwa na mahitaji makubwa ya vitabu katika shule zetu, vitabu
hivi vimewasili katika wakati mwafaka, na tunashukuru kwa msaada huu”,
na kungoeza kuwa juhudi kama hizi zitasaidia kuigeuza Zanzibar kuwa
jamii inayojitosheleza kiajira.
Alizitolea
wito shule zilizofaidika na vitabu hivyo kuvitumia vizuri kwa lengo la
kuisaidia Zanzibar kufikia malengo yake ya kielimu.
Bwana
Ame alimalizia kwa kuitolea wito ZADIA kupanua zaidi mfumo wa misaada
yake ya kielimu na kujumuisha ujenzi wa madarsa na vitabu vya taaluma
nyengine ambazo Zanzibar ina upungufu mkubwa, kama vile taaluma ya Fedha
na nyenginezo.
Naye
Mwenyekiti wa ZADIA Bwana Omar Haji Ali, alisisitiza azma ya Jumuiya
yake ya kuendeleza juhudi za kusaidia maendeleo Zanzibar.
Katika
hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na mwakilishi wa ZADIA Zanzibar
Bwana Mussa Shehe kwenye hafla ya makabidhiano ya vitabu hivyo, Bw. Ali
alisema “ZADIA, tangu kuanzishwa kwake imekuwa msitari wa mbele katika
harakati za kusaidia maendeleo Visiwani Zanzibar katika nyanja tofauti”
Aliendelea
kutamba kwa kusema kuwa, “Kwa vile ZADIA inaelewa kuwa daima maadui
wakubwa wa maendeleo ya jamii wamekuwa wakivinjari kuzorotesha maendeleo
hayo, basi jeshi letu siku zote liko imara kupambana na maadui hao
ambao ni maradhi, ujinga na umaskini, na kuhakikisha kuwa milele
hawatothubutu kujaribu kuyachokoza maendelea ya Wazanzibari.
Aidha,
Bwana Ali alisisitiza kuwa msaada huo wa vitabu siyo mwisho wa juhudi
za ZADIA katika kusaidia sekta ya Elimu Zanzibar, bali ni mwendeleo wa
mapambano dhidi ya adui ujinga.
Alielezea
matumaini yake kuwa msaada huu utakuwa ni changamoto kwa jumuiya
nyengine za Wazanzibari ulimwenguni kushiriki katika kusaidia maendeleo
Zanzibar.
Bwana
Omar aliwashukuru WanaZaida wote walioshiriki katika kufanikisha msaada
wa vitabu hivyo, pamoja na shirikika la Goodheart-Willcox la nchini
Marekani kwa ukarimu wao.
Hafla
hiyo ya makabidhiano ya vitabu, pia ilihudhuriwa na maofisa wa ngazi za
juu kutoka Wizara ya Elimu Zanzibar, Maofisa wa Idara ya Diaspora
katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar, wawakilishi wa Vyuo vilivyokusudiwa
kufaidika na msaada huo pamoja na wawalikishi wa vyombo mbalimbali vya
habari vilioko Zanzibar.
No comments:
Post a Comment