Ndugu Zangu,
Nilikuwepo
pale Viwanja vya Jangwani. Nilipomsikia Ben Mkapa akiwaita wapinzani '
Wapumbavu na Malofa', basi, nikajua hiyo ndio ingekuwa ' Habari ya
Mjini'. Nilikuwa sahihi. Ni kwa vile aliyetamka hayo alikuwa Ben, Rais
Mstaafu.
Na
hakika, mitaani huko nimekutana na watu wanaohangaika sana hata kuingia
kwenye kamusi ya Kiswahili kuona tafsiri ya maneno aliyotamka Ben, kama
ni matusi au la!
Katika
hili, yaweza pia kusemwa, kuwa Ben amechangia kupromoti lugha ya
Kiswahili. Na hakikatafsiri zaweza kuwa nyingi, na hasa katika wakati
huu wa joto la kisiasa linalopanda. Tukianza na Lofa, ina tafsiri ya mtu
aliyefilisika,kupungukiwa mtaji na hata mwenye kutembea akipoteza muda.
Yaweza pia kutafsiriwa kuwa kufilisika kisiasa. Inategemea na imetamkwa
katika muktadha gani. Chimbuko lake ni kwenye kimombo; ' wasting time'-
Are you loafing, you better hurry up and do! ....
Naam,
mapambano ya kisiasa, na hususan kwenye kampeni za uchaguzi huwa na sura
ya mikakati inayyofanana na ya mapambano ya kijeshi. Na kwenye vita
kinachopelekea ushindi ni vitu vitatu; Silaha bora, uwezo wa wapiganaji
na propaganda.
Huenda si
wengi wenye kukumbuka kuwa Ben Mkapa alipata kuwa Waziri wa Mambo ya
Nchi za Nje kwenye kipindi ambacho Tanzania ilikuwa vitani dhidi ya Idd
Amin.
Ni Ben
Mkapa aliyeongoza vita vya propaganda dhidi ya Idd Amin, dunia
ikaaminishwa kuwa Tanzania ilikuwa na sababu, uwezo na nia ya kumpiga
Idd Amin. Ni kwenye kipindi kile cha vita, na kazi ya fasihi kwenye
lugha ya vita ilifanywa na watu wa aina ya Ben Mkapa na Paul Sozigwa na
iliyotumika vema kwenye propaganda za kimapambano. Ndio, ikamfanya Idd
Amin aonekane si lolote si chochote.
Nini basi tofauti ya Mjinga na Mpumbavu?
Marehemu
Mzee Jongo alipata kutamka; ” Kusoma sio kuufuta ujinga, bali ni
kuupunguza”. Kila mwanadamu ana ujinga wa jambo moja au mia moja. Kuwa
na ujinga wa jambo si kosa, hata Profesa anaweza asijue namna ya
kuchochea kuni za kuchomea hindi bichi likachomeka. Kijana wa darasa la
saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda Profesa.
Lakini,
upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo isivyotakiwa huku akiwa
na uelewa wa namna ya kufanya inavyotakiwa. Huo ndio upumbavu.
Hoja ya
Ben kama ametukana au la, inabaki kuacha uwanja wazi wa tafsiri kwa
anayetaka kutafsiri anavyotaka yeye, bila kuacha kuzingatia, kuwa tumo
kwenye joto la kisiasa linalopanda. Na ndio utamu wa fasihi pia..!
Ukumbi wenu wajumbe kujadili.
No comments:
Post a Comment