Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), kimekata rufaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa majimbo ya Mlalo, Bumbuli, Ludewa na Peramiho yaliyotangazwa kuwa wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamepita bila kupingwa kwa madai kuwa waliotangaza hawana mamlaka hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Wakili wa Chadema, Peter Kibatala alisema tayari utaratibu wa kuandaa rufaa hizo umeshakamilika.
“Ninasimamia rufaa ya kesi tatu. Tunapinga wakurugenzi wa halmashauri kutangaza majimbo yao kuwa yana wagombea waliopita bila kupingwa wakati sheria haiwaruhusu kufanya hivyo.
“NEC pekee ndiyo wanaweza kusema lolote baada ya kusikiliza kilichoamuliwa na mkurugenzi,” alisema Kibatala.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa wagombea watano wa ubunge kupitia CCM wamepita bila kupingwa baada ya wawakilishi wa vyama vya upinzani kushindwa kujitokeza au kuwekewa pingamizi kutokana na makosa kadhaa ya kikanuni.
Mgombea wa Chadema Jimbo la Bumbuli, David Chanyezhea alisema baada ya kupokea barua ya kuenguliwa na mkurugenzi wa uchaguzi wilayani kwa maelezo kuwa amekosa vigezo, amekata rufaa NEC kupinga uamuzi huo.
Chanyezhea alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya jitihada za kumtaka ajiondoe kwenye kinyang’anyiro hicho na wapambe wa mgombea mwenzake wa chama kingine.
“Nimeshaandika barua ya kukata rufaa na kuituma NEC. Ninaamini haki itatendeka kwani sheria inaruhusu mtu kugombea udiwani na ubunge kwa wakati mmoja na wapo wabunge wa namna hiyo kwenye mabunge yaliyopita,” alidai mgombea huyo.
Hata hivyo, Wakili Kibatala alisema kutokana na makosa hayo, ana imani kuwa NEC itakuwa makini na kutoa majibu sahihi dhidi ya rufaa hizo.
Alipoulizwa kuhusu mustakabali wa majimbo mawili yaliyosalia, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema tayari hatua zimeshachukuliwa kwa lile la Peramiho na la Nanyamba.
Mwalimu alisema hawawezi kulizungumzia Jimbo la Nanyamba kwa kuwa mgombea aliyesimamishwa alikuwa wa CUF.
“Huko kwingine yalikuwa masuala ya kiufundi pekee ndiyo yaliyoleta changamoto, lakini hali imekuwa ya kushangaza kidogo… mgombea hakurudisha fomu,” alisema Mwalimu.
Taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo zilieleza kuwa kuna harufu ya rushwa kwenye jimbo la Nanyamba ambako mgombea wa chama hicho hakurejesha fomu na kumfanya yule wa CCM kukosa mpinzani.
No comments:
Post a Comment