Wagombea Chadema wadai kunasa kadi feki za mpigakura - LEKULE

Breaking

24 Aug 2015

Wagombea Chadema wadai kunasa kadi feki za mpigakura


Dar es Salaam.
Wagombea ubunge wa majimbo ya Kawe na Ubungo kwa tiketi ya Chadema, wamedai kubaini kadi 100 za wapigakura ambazo hazina taarifa.
Walidai jana kuwa kadi hizo ni mpango wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),  kujiandaa kuisaidia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Kailima Kombwey alisema hafahamu kuhusu kadi hizo, huku akishauri suala hilo lipelekwe polisi ili waliohusika wakamatwe.
Akizungumzia madai hayo katika mkutano na wanahabari, mgombea wa Ubungo, Saed Kubenea alidai, “Hapa tunazo 100, lakini tume imeandaa kadi kati ya 2,000 hadi 3,000 ambazo zitatumika kuwaandikisha wapigakura wengine kwa lengo la kuisaidia CCM.”
Aliwaonyesha waandishi wa habari kadi hizo, kisha kuziwasilisha kwa Wakili,  Frederick Kihwele aliyekuwapo katika mkutano huo.
Mgombea wa Kawe, Halima Mdee alisema uhakiki katika daftari la mpigakura unatakiwa kufanyika katika vituo vya kuandikisha kura badala ya kwenye ofisi za kata.
Alisema kata yenye watu 70,000, wananchi wake hawawezi kufanya uhakiki kwa siku nne zilizotolewa na NEC.
Mdee alidai kuwa wamepata taarifa kuwa wakimbizi 70,000 wameandikishwa kwa siri kwenye daftari hilo mkoani Kigoma.
Hata hivyo, Kombwey alisema hakuna mkimbizi aliyeandikishwa.
Akizungumzia siku za uhakiki katika daftari la mpigakura, Kombwey alisema suala hilo ni la kisheria na tume haiwezi kupingana nalo.

No comments: