Magufuli ataja vipaumbele 25 - LEKULE

Breaking

24 Aug 2015

Magufuli ataja vipaumbele 25


Dar es Salaam.
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amefungua pazia la kampeni za chama hicho kwenye Viwanja vya Jangwani katika tukio lililohudhuriwa na maelfu ya wananchi, huku akieleza mambo 25 atakayoyafanya iwapo Watanzania watamchagua kuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Huku akitumia maneno: “Mimi kazi tu”, “Tanzania ya Magufuli ni ya viwanda”, Dk Magufuli aliyetumia dakika 53 kueleza sera zake, kuanzia saa 11.40 hadi 12.33 jioni alisema Watanzania wanataka kitabu kipya cha mabadiliko na yeye na mgombea mwenza, Samia Suluhu ndiyo wanaoweza kuyaletea.
Dk Magufuli ambaye ni Waziri wa Ujenzi, alizungumza lugha za makabila saba kama ishara ya kuonyesha mshikamano wa Watanzania, huku makundi mbalimbali kama madereva, mama lishe na mengine yaliyokuwapo uwanjani hapo yakipaza sauti kutaka kusikia atawasaidia vipi akiingia Ikulu, ombi ambalo mgombea huyo aliwajibu na kutuliza kiu yao.
Mgombea huyo wa urais wa CCM aliahidi kuanzisha mahakama maalumu ya kusikiliza kesi za rushwa na ufisadi, kumaliza tatizo la wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo, kuhakikisha mama lishe hawabughudhiwi, kusimamia haki za wasanii, kulinda Muungano na usalama wa nchi.
Aliahidi kutoingilia utendaji kazi wa Bunge na Mahakama, kuheshimu mawazo ya vyama vingine vya siasa, kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara wadogo na wakubwa wote kulipa kodi, kuendeleza kilimo, mifugo, uchimbaji wa madini, majisafi na elimu bora.
Nyingine ni kusimamia nishati ya gesi, ujenzi wa barabara, reli, kuboresha sekta ya utalii, kuimarisha uwekezaji, kuwasaidia walemavu na kusimamia uhuru wa habari.
Mkutano huo ulioanza rasmi saa 9.30 alasiri ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Salim Ahmed Salim.

Ahadi alizotoa
Mgombea huyo alitoa ahadi mbalimbali ikiwamo ajira akisema: “Ninataka Watanzania wapate ajira, kazi ya Serikali itakuwa kukusanya kodi tu. Viwanda vinaweza kutengeneza ajira kwa asilimia 40 hasa kwa vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini.”
Kuhusu ubinafsishaji, alisisitiza: “Kuna viwanda vilibinafsishwa sasa wahusika wasipoviendeleza wajiandae kuvirudisha haraka.”
Mbali na kurejesha viwanda vilivyobinafsishwa, alisema akipewa ridhaa hiyo atahakikisha chini ya uongozi wake, anajenga viwanda vingi vipya, akiainisha vile mahsusi kwa shughuli za kilimo, mifugo, kusindika nyama na madini.
Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kilimo na kwamba atahakikisha sekta hiyo ambayo ndiyo mhimili wa uchumi inaendelezwa.
“Tutaleta vitendea kazi, pembejeo na vifaa vingi vya kisasa na vya kutosha kwa wakulima… kama nilivyosema hapo awali, tutajenga viwanda kwa ajili ya wakulima pia.
Mbunge huyo wa zamani wa Chato alisema pia kipaumbele kingine katika Serikali yake ni kuhakikisha kuwa wananchi wa mjini wanapata majisafi na salama kwa asilimia 95 na wananchi wa vijijini wanapata maji kwa asilimia 85.
Kuhusu afya alisema: “Tutahakikisha tunakuwa na vituo vya afya, zahanati na hospitali katika maeneo mbalimbali kwa sababu tunaamini maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana kama wananchi hawana afya bora.”
Kipaumbele kingine ni mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu akisema watakuwa wanapata mikopo kwa wakati bila kuchelewa na kwamba watajikita pia katika kujenga hosteli kwa wanafunzi wa vyuo.
“Mishahara ya walimu na wafanyakazi wote tutaishughulikia. Hata madereva haki zao za msingi lazima ziangaliwe,” alisema huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Mgombea huyo alisema anafahamu kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na kwamba maendeleo ya kweli yatapatikana kama changamoto hiyo itafanyiwa kazi.
“Tutaunganisha mikoa yote kwa barabara zenye viwango vya lami na pia tutajenga barabara za juu saba jijini hapa,” alisema Magufuli.
Alisema akipewa ridhaa hiyo itashughulikia suala la reli  kwa kujenga reli ya kisasa kwa viwango vya Standard Gauge” na kuboresha bandari na usafiri wa anga.
Kuhusu maliasili, alisema ni kipaumbele katika Serikali yake endapo akipewa ridhaa ya kuongoza nchi huku akieleza kukerwa na ujangili... “Ninapata shida sana ninapoona meno ya tembo yanauzwa Ulaya halafu unaambiwa yanatoka Tanzania… sasa unajiuliza yanapitaje?”
Alisema ili kushughulikia suala hilo atahakikisha watendaji wa sekta hiyo wanaboreshewa masilahi yao ili wachangie mapato ya nchi.
Aliahidi Serikali yake kuwa rafiki wa wawekezaji na kwamba italinda masilahi ya wafanyabiashara.
Mgombea urais huyo aliahidi kuwa atalinda uhuru wa habari na atafanya kazi na waandishi wa habari siyo tu wakati wa kipindi cha kampeni, bali hata baada.
Katika ahadi zake, Dk Magufuli hakuwaacha wasanii, alisema atahakikisha wanapata hakimiliki na kuhakikisha wao pamoja na wanamichezo wanaanzishiwa mfuko kwa ajili ya kuwasaidia katika mambo mbalimbali.
Dk Magufuli ambaye alirejea kauli yake; “naomba kazi ya urais kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania,” alisema itaimarisha vyombo vya ulinzi kwa kuwapa vifaa vya kisasa kwa ajili kuendesha shughuli zao.
Hata hivyo, alisema mabadiliko ya kweli hayawezi kupatika kama kutakuwa na matabaka kati ya Watanzania.
“Tutahakikisha kunakuwa na umoja wa kitaifa. Lazima watu wote wawe wamoja hakuna ukabila, udini… nimejiandaa kulinda umoja wa Watanzania wote,” alisema.
Aliahidi pia kulinda Muungano wa Tanzania na kuhakikisha ulinzi na usalama vinakuwa nguzo katika Serikali ijayo.

Azidisha muda
Kana kwamba alikuwa amenogewa kumwaga sera, Dk Magufuli aliyeanza kuhutubia saa 11.40 alimaliza saa 12.33 na hivyo kuzidisha dakika 33 katika muda unaoruhusiwa kikanuni na kwa mujibu wa ratiba ya kampeni.
Ilipofika saa 11.26 mwanajeshi mmoja alimfuata na kumnong’oneza kitu, jambo linadhaniwa kuwa alikwenda kumkumbusha kuhusu muda wa kampeni.
Akizungumzia suala la muda wa kampeni, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Kombwey alisema mikutano ya kampeni za uchaguzi inatakiwa kumalizika saa 12.00 jioni.
“Tumeweka kanuni zetu, mikutano ya kampeni za uchaguzi kwa vyama vya siasa itamalizika saa 12.00 jioni na si vinginevyo,” alisema.

Rais Kikwete amnadi
Akimtambulisha Dk Magufuli na mgombea mwenza Samia Suluhu alisema ndiyo wagombea sahihi wa kuliongoza Taifa.
Alisema Dk Magufuli ndiye mgombea pekee ambaye hana makundi kwa kuwa wakati wa mchakato wa kutafuta kuteuliwa na chama kugombea nafasi hiyo, alizunguka peke yake nchi nzima kutafuta wadhamini.
Kiongozi huyo aliendelea kubainisha kuwa Dk Magufuli ameweka rekodi nzuri katika nafasi mbalimbali alizowahi kushika akiwa serikalini. Alisema katika wizara tatu alizofanya kazi wakati wa utawala wake amefanya kazi nzuri ambayo ndiyo iliyompa sifa aliyonayo sasa.
“Kwenye sekta ya uvuvi, Dk Magufuli alikuwa anajua hadi idadi ya samaki katika Ziwa Victoria. Tukija sekta ya ardhi, yeye ndiye aliyesababisha kuwapo kwa kanda tulizonazo sasa, sekta ya ujenzi ndiyo usiseme, tuna barabara nzuri kila kona,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete aliwapongeza wakazi wa Dar es Salaam kwa kujitokeza katika viwanja vya Jangwani na kusema lazima wapinzani waogope.
Aliendeleza shutuma kwa wapinzani kuwa wanachukua picha za zamani ili ionekane kwamba kuna watu wengi waliohudhuria mikutano yao.
“Wanachukua picha za (Dk Willibrod) Slaa za wakati ule, wanaweka picha ya yule mzee ili ionekane wamevuta watu wengi kweli, watu wa ajabu sana,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa.
Alieleza kushangazwa kwake na upinzani kwamba amekuwa akifuatilia kwa kina ni jambo gani ambalo unalisimamia lakini hajaona hoja hata moja zaidi ya kutaka kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi.
“Kuna huyu mwingine alihama jana (Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye), yeye ndiyo sikumwelewa kabisa anasema nini, wanajichanganya tu. Hata ukiangalia mgombea wa urais wa upinzani (Edward Lowassa), anafuata sera za CCM, mgombea mwenza wake (Juma Duni Haji), anafuata sera za CUF,” alisema Kikwete na kusisitiza kuwa Dk Magufuli ndiye kiongozi bora anayefaa kuliongoza Taifa hili.
Alisema Tanzania inahitaji Rais anayewapenda Watanzania, hawataki Rais maskini lakini wanamtaka Rais ambaye hawana shaka na jinsi alivyozipata mali zake.
Alieleza mashabiki wa chama hicho kuwa ni mashahidi kuwa Dk Magufuli ni mwadilifu kwa sababu hakuwa na mtandao na Tanzania chini ya mikono yake itakuwa salama.

No comments: