Maalim Seif akabidhiwa fomu za urais Zanzibar, ailamu ZEC - LEKULE

Breaking

24 Aug 2015

Maalim Seif akabidhiwa fomu za urais Zanzibar, ailamu ZEC


Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad jana alichukua fomu kuwania urais wa Zanzibar, ikiwa ni mara ya tano, safari hii akiwa chini ya mwamvuli wa Ukawa.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, aliwasili Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) eneo la Bwawani akisindikizwa na viongozi wa ngazi za juu wa vyama vinavyounda Ukawa.
Waliomsindikiza Maalim Seif katika safari hiyo mbali na mamia ya wafuasi wake, ni pamoja na mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji.
Katika hafla hiyo, mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu, huku chama cha APPT – Maendeleo kikituma ujumbe wake katika hafla hiyo.

Mbali na kuungwa mkono na Ukawa, safari hii Maalim Seif yuko bega kwa bega na waliokuwa vigogo wa CCM wakiwa washauri na wasindikizaji wake.

Vigogo hao walioshuhudia akipokea fomu kutoka kwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha ni Mshauri wa Mkakati wa Ushindi, Mansour Yussuf Himid na mmoja wa waasisi wa CCM, Hassan Nassor Moyo.

Baada ya kuchukua fomu hiyo, Maalim Seif aliilaumu tume hiyo kuwa haijabadilika kwa kuwa haina uwazi wala umakini hasa kwa kushindwa kuweka bayana mipaka ya majimbo mapya ya uchaguzi yaliyoidhinishwa hivi karibuni.

Alisema hali hiyo inawachanganya na kuwanyima fursa ya msingi wapigakura na kuwapa shaka wananchi wa Zanzibar katika utekelezaji wa haki yao ya kidemokrasia.
Maalim alisema hata Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameshindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa mara tu alipotangazwa kushinda nafasi hiyo, Oktoba 31, 2010 ya kuirekebisha haraka sekretariati za tume hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari na baadhi ya wageni walioambatana naye katika hafla hiyo, Maalim Seif alitoa changamoto kwa wagombea wengine wa urais wa Zanzibar, akiwamo Dk Shein watamke na kukiri kwamba watakubali matokeo ya kushindwa iwapo uchaguzi huo utakuwa wa huru na haki.
Mbali na Maalim Seif na Dk Shein anayechukua fomu leo, wengine wanaowania urais Zanzibar ni Kassim Bakar Ali wa Jahazi Asilia na Abdalla Kombo Khamis wa DP.

Tumejiandaa
Maalim Seif alisema safari hii chama chake na safu yote ya upinzani wamejiandaa vya kutosha kwa ajili ya ushindi, licha ya kile alichokitaja kama hujuma, vitisho na mizengwe kutoka chama tawala.
Aliyataja mafanikio aliyoyapata katika ziara yake ya hivi mkoani Lindi kuwa alivuna zaidi ya wanaCCM 1,200 hatua ambayo ni dalili ya kuporomoka kwa chama hicho.
Kiongozi huyo alirejea kauli yake kuwa mara hii CUF haitakubali kupokwa ushindi endapo itashinda kihalali.

Aliahidi kwa niaba ya Ukawa kuwa, upinzani utafanya kampeni, kuanzia uzinduzi Agosti 29 jijini Dar es Dar es Salaam na Septemba 7,  Zanzibar kunadi sera na maendeleo na si fujo, matusi wala vinginevyo ili kushawishi na kuhakikisha umma wa Watanzania unaelekeza kura zao upande huo na kuleta ushindi wa kihistoria.

Katika mkutano huo, viongozi na wanachama wa CCM waliendelea kujiunga na upinzani akiwamo naibu waziri wa zamani wa Mawasiliano Zanzibar, Mohamed Hashim Ismail ambaye tayari ameteuliwa na CUF kugombea uwakilishi Jimbo la Dimani.

No comments: