Wasomi: Sumaye ataimarisha upinzani - LEKULE

Breaking

24 Aug 2015

Wasomi: Sumaye ataimarisha upinzani


Dar es Salaam.
Wasomi mbalimbali nchini wamesema kitendo cha Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kuhamia upinzani kutakiathiri Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ya nguvu ya ushawishi aliyonayo katika jamii.

Juzi, Sumaye alitangaza kuihama CCM na kujiunga na upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa kile alichoeleza kuwa ni kutaka kuimarisha upinzani na kujenga chama mbadala ambacho wananchi wanaweza kukichagua.

Hatua hiyo ni mfululizo wa wanachama wa CCM kuhamia upinzani kwa madai ya kutoridhishwa na mchakato wa kuwapata wagombea katika nafasi mbalimbali za urais na ubunge.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema hatua hiyo ya Sumaye hiyo ni ishara kuwa chama hicho kimepoteza mvuto kwa watu wake.
Alisema ilizoeleka kwamba wapinzani ndiyo waliokuwa wakikikosoa chama hicho tawala kutokana na mfumo wake mbovu wa kiutawala, lakini wanapohama vigogo wake, wanatia msisitizo kuhusu ubovu huo.

“Kuhama kwa Sumaye kunashawishi pia wananchi kwa sababu alikuwa kwenye mfumo wa utawala. Pia, kutaathiri upigaji kura dhidi ya CCM. Kwa hiyo, hilo siyo jambo dogo kwa CCM,” alisema.
Profesa Mpangala alisema katika siasa, kuna wakati kinakuja kimbunga cha watu kutaka mabadiliko. Alisema hiki ni kimbunga cha mabadiliko ambacho kitaufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa na ushindani mkubwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema Sumaye alikwa na nafasi kubwa serikalini na ndani ya chama, hivyo lazima athari ziwepo kwa sababu kimepoteza mtu muhimu ambaye angesaidia kumnadi mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli.
Alisema Sumaye anajua mambo mengi ya chama chake na siri zilizokifanya kiendelee kutawala na kwamba atatumia ujuzi huo kuusaidia upinzani kushinda kwenye uchaguzi wa Oktoba 25.
“Uchaguzi huu utakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu wananchi wameamka na upinzani umeimarika. Hakuna upande wa kumbeza mwenzake, hapa ni kufanya siasa kwa umakini mkubwa,” alisema Salim.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana alisema Sumaye hakuwa na nafasi yoyote ndani ya chama tangu alipoondoka madarakani mwaka 2005, hivyo hakuna athari zozote kwa CCM.

Dk Bana alisema Sumaye hakupata washauri wazuri na wapo mawaziri wakuu wastaafu waliokuwapo kabla yake lakini wamekuwa wakikikosoa chama kupitia vikao vya ndani.
Lakini mhadhiri mwenzake Udsm, Dk Lupa Ramadhan alisema: “Kwa wabunge ni kitu cha kila siku. Anaweza akahama hata vyama viwili au vitatu kwa msimu mmoja wa uchaguzi na wala isiwe habari kubwa lakini inapotokea viongozi wakubwa kama Sumaye ni jambo linaloongeza kasumba ileile ya wanasiasa. Ni katika kutekeleza haki yake ya kidemokrasia.”

Mhadhari mwingine wa chuo hicho, Charles Kayoka alisema Ukawa inajiongezea mtaji wa watu wenye mvuto na hali hiyo itaimarisha demokrasia za ndani na kuifanya siasa kuwa ya kuvutia zaidi. “Marais waliopita pamoja na (Jakaya) Kikwete wanastahili pongezi kwa hili. Hivi sasa itakuwa si ajabu kwa mtu yeyote kuwa katika chama chochote cha siasa tofauti na zamani na aliyekorofishana na CCM alipaswa kuhama nchi.
Tunakoelekea hatutakuwa na vyama vya upinzani, bali vyote vitakuwa vyama vya siasa vyenye ukubwa sawa,” alisema.

No comments: