WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ametangaza rasmi kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga kwenye vuguvugu la mabadiliko kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Sumaye
ametangaza uamuzi huo leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Legde Plaza
uliopo katika Hoteli ya Bahari Beach Jijini Dar es Salaam.
“Leo
nimeamua kuondoka CCM na kujiunga na UKAWA, uamuzi huu haukuwa rahisi
katika familia yangu…, suala la kujiunga na chama gani itajulikana
baadaye,” amesema.
Amesema, atasaidiana na Edward Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chadema na pia mwakilishi wa UKAWA kufanikisha mageuzi.
UKAWA unaundwa na vyama vinne vya upinzani ambavyo ni Chadema yenyewe, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na NLD.
Sumaye
amesema, Lowassa amekaa kwenye nafasi mbalimbali za utawala ndani ya
serikali hivyo anastahili nafasi hiyo na kwamba, hana tatizo na utendaji
wa mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Mgufuli lakini sio katika ngazi
ya urais.
“Sina tatizo na Magufuli, naamini hakuhonga na ni mchapakazi lakini ana mapungufu mengi katika nafasi hiyo (urais),” amesema.
Mkutano
huo wa Sumaye na waandishi wa habari pia umehudhuriwa na Lowassa,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia, Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Siasa na Bunge wa CUF, Shaweji
Mketo na viongozi wengine wa UKAWA.
Tayari
Lowassa na mgombea mwenza wake Juma Duni Haji jana wamerudisha fumu za
kugombea urais kwenye Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC) na kukidhi vigizo
vilivyowekwa.
Hatua
ya Sumaye kuhama CCM inakuja ikiwa ni siku moja kabla ya Dk. Magufuli
kufungua rasmi kampeni ya chama chake kuelekea Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Kwenye
mkutano huo Sumaye ambaye aliongozana na mkewe Esther Sumaye pamoja na
wana familia wengine amesema, anaondoka kwenye chama hicho ili kuongeza
nguvu ya upinzani.
“Siji upinzani kufuata cheo, nakuja kuimarisha nguvu. Sijadai cheo wala fedha. Nipo tayari kusaidia upinzani ili uwe na nguvu,” amesema Sumaye na kuongeza:
“CCM
imezubaa, inajifanya itashinda. Wananchi wanataka mabadiliko na
hatuwezi kuwaacha hivi hivi, sisi wenye uchungu na nchi hii hatuwezi
kuwaacha hivi hivi. Nimekuja huku ili kuongeza nguvu ya mabadiliko.”
Hata
hivyo Sumaye amewataka wanachama wa CCM pamoja na watumishi wa serikali
walio tayari pia wajiunge na UKAWA ili kuhakikisha wimbi la mageuzi
linafanikiwa.
“Mimi
sijui kama ni mmoja wa wale walioitwa makapi, ningejua ningetoka
mapema…, sitoki CCM kwa hasira ya kutoteuliwa, kumchukia mgombea urais
wa CCM, kuchukia uongozi wa juu wala kudhoofisha CCM, badala yake natoka
ili kuimarisha CCM,” amesema.
Akifafanua
kauli hiyo amesema kuondoka kwake CCM na kuimarisha nguvu ya UKAWA
kutaisaidia CCM kutolala na kuongeza nguvu ili kupambana na vyama vya
upinzani.
Amesema,
wana CCM hawapaswi kusikitika kwa yeye kuhama chama hicho kwani ni mtu
wa kawaida ndani ya chama hicho na kwamba, hana cheo chochote.
“Wana CCM hawana sababu ya kulalamika, mimi ni sisimizi ndani ya CCM, sina nafasi yoyote hata ujumbe wa tawi,” amesema na kuongeza, chama hicho hakikuona umuhimu wake na pengine kitauona baadaye.
Hata
hivyo Sumaye amesema, hakuhama kwa sababu ya kumfuata Lowassa kwa kuwa,
ametoka Kaskazini, “lakini pia si kwa sababu Mbowe ni mtu wa
Kaskazini,” isipokuwa ni kuimarisha mageuzi.
Hata hivyo ameoneshwa kutishwa na wimbi la mageuzi nchini na kusema “wimbi hili kulizuia si kazi rahisi.”
Sumaye
ameshutumu vikali hatua ya wachache kuharibu taratibu za CCM katika
kupata mgombea urais kupitia chama hicho na kuwa, alijua mapema kwamba
jina lake halitafika mbali.
Anasema,
hana tatizo na mfumo wa kupata wagombea isipokuwa tabia ya watu
wachache kwenda na majina ya wagombea kinyume na taratibu za chama.
“Katika
mfumo huu mtu mwenye nafasi ya juu na anataka akuingize anaweza kufanya
hivyo na kama hataki anakuondoa. Mfumo huu ni mbuvu, safari haya
yametokea sana.
“Rais,
katibu mkuu hana nafasi ya kuweka mgombea. Rushwa ni tatizo ndani ya
CCM, ukipinga rushwa unaonekana tatizo ndani ya CCM. Hili
linathibitika,” amesema.
Hata
hivyo ameshauri wale walio na mtazamo kwamba, nje ya CCM hakuna maisha
ya siasa wabadilike maana mawazo hayo yamepitwa na wakati.
No comments:
Post a Comment