Wasanii Wageukana kwa Rais Kikwete - LEKULE

Breaking

22 Aug 2015

Wasanii Wageukana kwa Rais Kikwete


WIKI chache zilizopita wasanii waliandaa tafrija ya kumuaga Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa nao bega kwa bega tangu alipoingia madarakani mwaka 2005 akiwasaidia kwa mambo mengi.

Hafla hiyo ilifanyika Mlimani City, sasa sikia kilichojiri baada ya shughuli hiyo kufanyika.

Umoja wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania umeibuka na kuwacharukia wenzao walioratibu hafla hiyo wakidai kuwa hawakuwa na uhalali wowote kwani umoja wao hautambuliki kisheria, hivyo halikupaswa kuwawakilisha wasanii wote.

Mashirikisho ya Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), la Filamu Tanzania (TAFF), la Sanaa za Maonesho Tanzania (TAPAF) na la Muziki Tanzania (TMF), yamedai waliibiwa wazo lao hilo walioliibua miezi miwili iliyopita kabla ya kupigwa bao na wenzao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mashirikisho hayo, Kimella Billa, akizungumza kwa niana ya marais wa umoja huo, alisema wanatambua haki ya watu au makundi tofauti katika kuandaa shughuli na matukio mbalimbali likiwemo kumuaga Rais Kikwete, lakini kilichofanywa na wezao si sahihi.

“Tunachopinga hapa ni namna ambavyo watu hao wasiyo na nia njema na tasnia ya sanaa, kutumia mwamvuli wa wasanii wote kinyume cha utaratibu. Ikumbukwe kwamba sanaa nchini ni pana kuliko uwakilishi wa kibaguzi ulifanywa katika tukio tajwa,”alisema Billa.

“Hivyo tukio lile siyo tu limekiuka matakwa ya kisheria kwa kutumia jina ambalo halijasajiliwa, bali waandaaji walimdanganya Rais kwa kujifanya wao ndiyo wawakilishi halali wa wasanii nchini, lakini pia limeleta sintofahamu na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wasanii wote,” alisema.

Nikki wa Pili akizungumza kwa niaba ya walioandaa halfa hiyo, alikiri kuwa umoja wao haupo rasmi, lakini unaundwa na wasanii rasmi ambao wamekuwa wakifanya shughuli zao mbalimbali kwa pamoja na kufanikisha.


Katibu wa BASATA, Godfrey Mngereza ameeleza kikundi cha Muungano wa Wasanii nchini ulioandaa hafla hiyo ya kumuaga Rais Kikwete hakijasajiliwa.

No comments: