Rufaa za Mramba, Yona kutolewa uamuzi Septemba 18 - LEKULE

Breaking

7 Aug 2015

Rufaa za Mramba, Yona kutolewa uamuzi Septemba 18


UAMUZI wa rufaa mbili za kupinga adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh milioni tano, zilizowasilishwa na Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona pamoja na upande wa Jamhuri, unatarajiwa kutolewa Septemba 18 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika rufaa hizo, Mramba ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wanapinga hukumu iliyotolewa Julai 6, mwaka huu na jopo la Mahakimu watatu, likiongozwa na John Utamwa. Wengine ni Saul Kinemela na Sam Rumanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mawaziri hao walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini hiyo, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7. Jaji Projest Rugazia alitoa tarehe hiyo juzi baada ya mawakili wa pande zote mbili kukubaliana kuwasilisha hoja za rufaa hizo mbili kwa njia ya maandishi.

Akiahirisha rufaa hiyo, Jaji Rugazia alisema pande zote mbili ziwasilishe hoja Agosti 12, mwaka huu, majibu yawasilishwe Agosti 19, mwaka huu na hukumu itatolewa Septemba 18, mwaka huu.

Jaji Rugazia anatarajia kutoa uamuzi dhidi ya adhabu ya Mramba na Yona pamoja na kuachiwa huru kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, ambapo wote kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.

Mawaziri hao wamekata rufaa kwa madai kuna upungufu kwenye mwenendo wa kesi iliyowatia hatiani, kwa kuwa hati ya mashitaka ilikuwa na kasoro, haikuwa sahihi. Aidha ushahidi wa upande wa Jamhuri haukuwa na uzito wa kuwatia hatiani, adhabu iliyotolewa ilikuwa kubwa. Pia hawakuridhika na uendeshwaji wa kesi hiyo.

Kesi hiyo ilikuwa inawakabili watu watatu lakini, Mahakama ya Kisutu ilimuachia huru Mgonja baada ya kumuona hana hatia. 
 
Hata hivyo, upande wa Jamhuri pia umekata rufaa kupinga adhabu iliyotolewa dhidi ya mawaziri hao ambao kwa sasa wanaendelea kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Wanadai kuwa hawajaridhika na uamuzi uliotolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.


Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mwaka 2008 wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.

No comments: