CHAMA
cha ACT – Wazalendo kimesema hadi sasa wamejitokeza wagombea katika
majimbo 203 ya uchaguzi nchini huku kura za maoni za kupata wagombea
katika majimbo mbalimbali zikiendelea.
Kwa
mujibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba, hadi kufikia
Ijumaa iliyopita, chama hicho cha upinzani nchini kilikuwa na wagombea
298 katika majimbo 203 nchini kati ya majimbo 265 yaliyopo.
Mwigamba
aliuambia mtandao huu kuwa chama hicho ambacho Kiongozi Mkuu wake ni
aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, Zitto Kabwe,
kitasimamisha mgombea kwa kila jimbo la uchaguzi nchini.
“Chama
chetu kitasimamisha mgombea katika kila jimbo nchini.Na hadi kufikia
Ijumaa iliyopita, tulikuwa na wagombea 298 katika majimbo 203. Kwa sasa
kura za maoni zinaendelea katika sehemu mbalimbali nchini na baadhi yao
wamekwisha kamilisha uteuzi wa wagombea,” alisema Mwigamba.
Alitaja
baadhi ya majimbo yaliyopata wagombea kuwa ni Kigoma Mjini ambako
ameshinda Zitto, Kasulu Mjini alikoshinda aliyekuwa Mbunge kwa tiketi ya
NCCR-Mageuzi, Moses Machali na Kasulu Vijijini ambako ameshinda Thomas
Matatizo ambaye ni mwanasheria wa chama hicho.
Alisema
majimbo mengine yalitarajiwa kufanya kura za maoni jana ikiwamo Singida
Mjini ambako anagombea Mwenyekiti wa Taifa wa ACT – Wazalendo, Anna
Mghwira, huku majimbo mengine yakitarajiwa kufanya leo na kesho ikiwamo
Ubungo ambalo litafanya kesho na ambako Mwigamba amejitosa kuwania
uteuzi huo.
“Majimbo
mengine yanaendelea na kura za maoni kwa sasa. Kwa mfano, Tarime Mjini,
Tarime Vijijini, Bukombe, Singida Mjini yanatarajiwa kufanya kura hizo
kati ya leo (jana) na kesho (leo). Geita Mjini walifanya, lakini
kulitokea ukiukwaji wa taratibu na wakaomba zoezi hilo lilirudiwe,” alieleza Mwigamba.
Aidha,
alisema wanaendelea kupokea baadhi ya wanachama waliokuwa katika vyama
vingine vya upinzani ambao wanajiunga na chama hicho, akitaja baadhi yao
kuwa walikuwa wagombea katika majimbo ya Musoma Mjini, Bunda Mjini,
Tarime Mjini (wote wametoka Chadema) na Mtama (ametoka CCM).
Kuhusu
wagombea wa urais, alisema hadi sasa amejitokeza mgombea mmoja, ingawa
wapo wanawake wawili walioonesha nia lakini hawajachukua fomu ambazo
zitatolewa mpaka Agosti 11, mwaka huu.
Katibu
Mkuu huyo wa ACT – Wazalendo alisema vikao vya uteuzi vitaanza Agosti
12 kwa kukutana na Sekretarieti itakayofuatiwa na Kamati Kuu Agosti 14,
Halmashauri Kuu ya Taifa Agosti 15 na Mkutano Mkuu utafanyika Agosti 16,
mwaka huu kupitisha Mgombea wa Urais na kufanyia marekebisho Ilani ya
Uchaguzi ya chama hicho.
ACT
- Wazalendo ilipata usajili wake wa kudumu Mei, 2014, na mapema mwaka
huu, Zitto alijiunga nacho na kutangazwa kuwa Kiongozi Mkuu. Ni chama
kinachoamini katika misingi ya Ujamaa Demokrasia.
No comments:
Post a Comment