Maalim Seif Amlipua Profesa Lipumba........Asema Wanachama Waliojiunga CUF Kwa Sababu ya Lipumba Wanaweza KUONDOKA Pia - LEKULE

Breaking

8 Aug 2015

Maalim Seif Amlipua Profesa Lipumba........Asema Wanachama Waliojiunga CUF Kwa Sababu ya Lipumba Wanaweza KUONDOKA Pia


Wafuasi  wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na pia mwenyekiti mwenza wa muungano wa wapinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba, wameanza kushughulikiwa na kutakiwa kuchagua moja; kuendelea kuwa ndani ya chama hicho au kutoka.

Ingawa Profesa Lipumba alipojiuzulu uenyekiti, alisema ataendelea kuwa mwanachama wa CUF, lakini Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wanachama waliokuwa wakimuunga mkono, kuamua moja, kubaki ndani ya chama hicho kama alivyoamua mchumi huyo mashuhuri duniani, au kutoka.

“Profesa Lipumba kajiuzulu CUF, wale waliojiunga CUF kwa sababu ya Profesa, wanayo fursa ya kuamua kubaki CUF au kutoka,” alisema Hamad juzi usiku.

Mbali na kuwataka wanaomuunga mkono Profesa Lipumba kuamua kutoka ndani ya chama hicho au kubaki, wakati kiongozi wao akiwa ameweka wazi kuwa hana nia ya kutoka katika chama hicho, Maalim Seif alitoa kauli zingine kuashiria kutohitaji hata uanachama wa Lipumba ndani ya CUF.

“Kama ni treni inayokwenda Mwanza, ikifika Morogoro abiria watashuka, lakini wengine watapanda, ikifika Kaliua watashuka abiria lakini wengine watapanda,” alisema Maalim Seif alipofanya ziara ya ghafla katika Makao Makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam juzi usiku.

Hamad amewahakikishia wanachama wa chama hicho waliokuwa wamezingira ofisi hiyo, kuwa uamuzi wa Profesa Lipumba kujiuzulu wadhifa wake hautausambaratisha Ukawa na CUF, ambayo kwa sasa haina Mwenyekiti wala Makamu Mwenyekiti, lakini akasema imeendelea kubaki katika mikono salama.

Alisema akiwa Katibu Mkuu na viongozi wenzake waliobaki, watahakikisha kwamba chama hicho kinafikia malengo ya kuanzishwa kwake, ambayo ni kuhakikisha kinakamata dola.

Alisema mwishoni mwa wiki hii, chama hicho kitaanza vikao vyake kuzingatia hatua iliyotokea, ili wachukue uamuzi thabiti wa kukiongoza chama hicho na kuhakikisha kinabaki katika mikono salama, hadi hapo uchaguzi wa kumtafuta Mwenyekiti utakapofanyika.

Akizungumzia Ukawa, Hamad alisema baada ya hatua hiyo ya Profesa Lipumba, alizungumza na viongozi wakuu wa umoja huo, akiwemo Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) na Emmanuel Makaidi (Mwenyekiti wa NLD) pamoja na mgombea urais wa umoja huo, Edward Lowassa na wamehakikishiana kuwa hawatarudi nyuma.

“Tumehakikishiana kwamba Ukawa upo na umeimarika zaidi na hatutarudi nyuma… Tumeona kwa namna unavyoungwa mkono na wananchi walio wengi, Magufuli (mgombea urais wa CCM) Ikulu ya Magogoni hataiona,” alidai Maalim Seif.

No comments: