MKAZI wa Kijiji cha Ishunju, wilayani Missenyi, Sikitu Filemoni (27), amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kutiwa hatiani kwa kumsababishia mwenzake ulemavu wa kudumu.
Hukumu hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Gera, Allen Ifunya, ili iwe fundisho kwa mshitakiwa na watu wengine wanaoshindwa kutawala hasira zao.
Ilielezwa mshitakiwa alimrukia Dafroza Severian (41), mkazi wa kijiji hicho na kumng’ata mdomo, kitendo kilichosababisha kuondoa kipande cha mdomo wa chini, hivyo kupata ulemavu wa kudumu.
Ilielezwa mahakamani kuwa, Agosti 4 mwaka huu, wanawake hao walikuwa wakibishana kuhusu matokeo ya kura ya maoni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyofanyika Agosti Mosi, ikuhusu udiwani katika Kata ya Ishunju, ambapo mgombea aliyekuwa akipendwa na mshitakiwa alishindwa, hivyo kujihisi kuwa anazomewa na mwenzake, ndipo alipomrukia na kumng’ata.
Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikiri kutenda kosa hilo.
Hakimu alimhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, adhabu itakayoanza kutumikiwa baada ya kuthibitishwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya.
Katika matokeo ya kura ya maoni ya udiwani kwenye kata hiyo, Msafiri Nyema maarufu Matelefoni, aliibuka mshindi kwa kupata kura 477, akiwabwaga Murshid Ibrahim (388) na Vincent Kamugisha (190).
No comments:
Post a Comment