SIKU chache baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Kawawa kushindwa katika kura za maoni ya ubunge ndani ya CCM katika Jimbo la Liwale mkoani Lindi, kaka yake, Vita Kawawa naye ameripotiwa kuanguka katika kura za maoni jimboni Namtumbo, Ruvuma.
Vita (51) aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 2005, amezidiwa nguvu na washindani wake, Edwin Ngonyani aliyeongoza kwa kupata 12,606 na Salome Sijaona aliyeshika nafasi ya pili kutokana na kura 7,002.
Kwa mujibu wa Juma Mpeli, Katibu wa CCM Songea Mjini aliyesimamia kura hizo kutokana na Katibu wa Namtumbo, Aziz Fakir kwenda kuwania ubunge Songea Mjini, Vita amepata kura 2,749 na hivyo kushika nafasi ya tatu.
Mpeli alisema uchaguzi huo ulikuwa marudio, baada ya ule wa awali uliompa ushindi mbunge huyo kuonekana kuwa na hitilafu. Wengine na kura zao baada ya marudio ya kura ni Fintan Kilowoko (1,959), Mussa Chowo (1,229), Mwenyeheri Ndimbo (939) na Ally Mbawala (452).
Mbali ya Vita, madiwani 18 pia wameripotiwa kuanguka katika kura za maoni, akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Steven Nana.
Nako katika Jimbo la Tunduru Vijijini ambako pia kulikuwa na hitilafu katika kura za maoni, mbunge wa jimbo hilo, Ramo Makani ameibuka mshindi.
No comments:
Post a Comment