Chama cha Wananchi (CUF), kimepinga amri ya jeshi la polisi ya kupiga marufuku maandamano nchi nzima, na kulitaka lijipange kuyalinda katika kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu.
CUF imetoa kauli hiyo baada ya wiki iliyopita Kaimu Mkuu wa Polisi, Abdurahman Kaniki, kutangaza kuzuia maandamano nchi nzima hadi uchaguzi upite kwa sababu za kiusalama.
Akijibu kauli ya polisi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Magdalena Sakaya, alisema jeshi hilo linatumiwa na CCM ili kufanikisha bao la mkono walilojinadi nalo mwaka huu.
Sakaya alisema maandamano ni haki ya Mtanzania kikatiba kama njia ya kujielezea na kulitaka jeshi hilo, kujiandaa kuyalinda kwa sababu ni jukumu lao.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 ibara ya 18 (a), kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake.
Pia alisema Ibara ya 20 (1) inasema, kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine.
Alisema ibara hiyo inaendelea kueleza kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na chama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengine.
Kadhalika, alisema sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2002 ibara ya 11 inatambua maandamano na mikusanyiko kama sehemu ya shughuli za vyama vya siasa.
“Haiwezekani leo watu wafanye kampeni za uchaguzi kimya kimya ni utamaduni ambao hata nchi zilizoendelea uliwashinda. Huwezi tenganisha kuandamana na kampeni za uchaguzi,” alisema.
Sakaya alisema kauli hiyo ya polisi ni dalili kuwa linatumiwa na CCM hasa baada ya kukosa umati mkubwa wakati mgombea wao akienda Nec kuchukua fomu.
Alisema tangazo la polisi ni batili na kwamba chama chao pamoja na Ukawa hawatalifuata.
Kuhusu kauli ya jeshi la polisi waliyoitoa juzi kuwa, watafanya utaratibu wa kukutana na wadau wa siasa ili kuzungumzia hilo, Sakaya alisema endapo jeshi hilo litaendeleza msimamo huo, wao hawataufuata.
Alisema kitendo wanachokifanya ni kuwatishia wananchi ili kupunguza ari ya kushiriki katika uchaguzi na kwamba ni dalili kuwa jeshi hilo limejiandaa kuleta vurugu na kuufanya uchaguzi kutokuwa huru na wa haki.
No comments:
Post a Comment