Rais Kikwete Atetea Uteuzi wa Dr. Magufuli Kugombea Urais........Magufuli Naye Arusha Dongo, Asema CCM Sio Safari ya Matumaini bali Ya Uhakika - LEKULE

Breaking

17 Aug 2015

Rais Kikwete Atetea Uteuzi wa Dr. Magufuli Kugombea Urais........Magufuli Naye Arusha Dongo, Asema CCM Sio Safari ya Matumaini bali Ya Uhakika



Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema uamuzi wa nani agombee urais kupitia chama hicho ulifanyika kwa pamoja na kufuata taratibu, hivyo anayetoka katika chama hicho kwa sasa ni kwa hiari na mapenzi yake.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema uamuzi huo ulifanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM na ulipigiwa kura ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya mjadala mrefu ambako uamuzi ulichukuliwa kwa pamoja.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni majibu ya matamko ya hivi karibuni ya wanaCCM wanaotoka katika chama hicho na kujiunga na vyama vinavyounda Ukawa, hasa Chadema, wakisema ni kutokana na kuvunjwa utaratibu katika mchakato wa kumpata mgombea urais, uliompitisha Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.

Miongoni waliotoka katika chama hicho tawala ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa pamoja na wenyeviti watatu wa mikoa ya Arusha, Singida na Shinyanga; Onesmo Ole Nangole, Mgana Msindai na Hamis Mgeja.

Katika majibu hayo, Rais Kikwete alisema hakuna haki iliyovunjwa katika mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM kwa sababu taratibu za chama hicho zinajulikana wazi na ni zilezile.

Badala yake, alisema mpango wa kukihama chama hicho ulikuwa umepangwa: “Ukweli ni kwamba baadhi ya watu walikwishaamua kutoka CCM hata kabla ya vikao vya Dodoma kuanza.”

Rais Kikwete aliwaambia vijana hao: “Aliyetoka, katoka mwenyewe kwa uamuzi wake mwenyewe lakini pale tuliamua wote. Maana pale tulipokubaliana kupiga kura, tulikubaliana kupiga kura kwa majina yale matano, siyo uamuzi wangu pekee yangu, bali ulikuwa uamuzi wa sote. Maana tulijadiliana na kukubaliana kwamba kwa mujibu wa katiba yetu majina ni hayahaya. Tukapiga na kura yakaisha.”

Alisisitiza: “Hivyo, anayetoka, anatoka kwa hiari yake mwenyewe kwa sababu pale Dodoma sote tulikubaliana… na kwa kweli wote wanaotaka kutoka ndani ya CCM wanatoka kwa hiari yao wenyewe na wala siyo kwa sababu ya kunyimwa haki.

“Sasa mchakato umekwisha. Aliyepata kapata. Aliyekosa kakosa. Mchakato huo haurudiwi tena,   hatuwezi kuitisha tena mkutano mkuu. Lililobakia sasa tunasubiri sasa Ndugu Magufuli arudishe fomu na baada ya hapo ni Iyena Iyena na mambo yanakwenda. Haya ndiyo mapenzi ya Mungu.”

Katika mchakato huo wa Dodoma, CCM ilimteua Dk Magufuli kuwa mgombea urais na Lowassa ambaye jina lake lilikatwa katika hatua za awali alihamia Chadema ambako pia chama hicho kikishirikiana na vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kimempitisha kuwania urais.

Magufuli aanza vijembe
Katika mkutano huo, Dk Magufuli alisema baadhi ya wapinzani ni waigizaji wakubwa ambao wamesomea uigizaji na wataufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kutawaliwa na mbwembwe na maigizo mengi.        

Alisema kazi kubwa ya CCM ni kukabiliana na mbwembwe na maigizo hayo ili kuyashinda.

Magufuli alisema CCM siyo watu wa matumaini, bali ni watu wa maendeleo na safari ya uhakika.

Alisema wapinzani wa CCM sasa wameanza kunukuu kila kitu hasa nyimbo za chama.

Aliwaambia vijana hao: “Katika mchakato huu na katika uchaguzi wa mwaka huu kuna mbwembwe nyingi, kuna mbinu nyingi na kuna maigizo mengi hasa kwa sababu wako wengine walisomea maagizo. Kwa hiyo tuna wajibu wa pamoja kuyashinda haya maigizo.”

No comments: