Baada ya Kujivua Uenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba Kajificha Burundi - LEKULE

Breaking

9 Aug 2015

Baada ya Kujivua Uenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba Kajificha Burundi


Aliyekuwa  Mwenyekiti  wa  Chama  cha  Wananchi (CUF),Profesa Ibrahim Lipumba  amesafiri  kutoka  jijini  Dar  es  Salaam  hadi  nchini  Burundi  kwa  shughuli  ambazo  hazijafahamika  wazi.

Profesa  Lipumba  aliondoka  Dar  es  Salaam, Alhamisi  ya  Agosti 6 mwaka  huu  kwa  ndege  ya  shirika  la  ndege  la Rwanda (Rwanda Air), huku  ikiwa  haijulikani  alikoelekea  muda  mfupi  baada  ya  kutangaza  kujiuzulu  wadhifa  wake  wa  uenyekiti  wa  CUF, kwa  kile  alichodai  kutoaminiwa  na  wenzake  ndani  ya  chama  pamoja  na  kutofautiana  mtazamo  na  msimamo  na  Viongozi  wa  Umoja  wa  Katiba  ya  Wananchi (UKAWA).

Uchunguzi  uliofanywa  na  mtandao  huu  tangu  kuondoka  nchini  kwa  Profesa  Lipumba, umeonyesha kuwapo  kwa  upotoshaji  wa  makusudi  wa  mahali  aliko  sasa,na  kwamba  hata  kabla  ya  kuondoka,  kulikuwa  na  jitihada  kubwa  za  kuficha  mwelekeo  wa  safari  yake.

Katika  uwanja  wa  ndege  wa  kimataifa  wa  Julius  Nyerere(JNIA)  Dar  ambapo  Lipumba  alifika  saa  saba  mchana  siku  ya  alhamisi  na  kuonwa  na  baadhi  ya  watu  waliohojiwa  na  mtandao  huu,alifika  eneo  hilo  akiwa  amevaa  suti  ya  rangi  ya  bluu  iliyokoza  na  shati  jeupe.

Baadhi  ya  watu  wake  wa  karibu  waliohojiwa  kuhusu  safari  yake  hiyo,walieleza  kuwa  alipanga  kusafiri  kwa  ndege  ya  shirika  la  Kenya (Kenya  Airways-KQ 485),lakini  mashuhuda  waliokuwa  uwanja  wa  ndege  walieleza  kuwa  hakusafiri  na  ndege  hiyo.

Mashuhuda  hao  walieleza  kuwa  Profesa  Lipumba  alifika  uwanjani  hapo  akiwa  na  walinzi  wawili  na  akiwa  mwingi  wa  wasiwasi,huku  macho  yake  yakiwa  yameiva  kwa  wekundu, na  aliondoka  na  ndege  ya  Rwanda  Air  saa  tisa  alasiri.

Taarifa  zilizopatikana  muda  mfupi  baada  ya  kuondoka,zilieleza  kuwa  alitua  Rwanda  na  baadaye  aliruka  tena  kuelekea  Uswisi.Lakini  baadaye  ilidaiwa  kuwa  alisalia  nchini  Rwanda  huku  ikiwa  haijulikani  shughuli  aliyokuwa  akiifanya.

Baadhi  ya  wanachama  wa  CUF  waliozungumzia  kuondoka  kwake,walihoji  namna  safari  hiyo  ilivyoandaliwa,huku  wakihusisha  kuwa  na  msukumo  wa  wanasiasa  wenye  nguvu  hapa  nchini.


Hata  hivyo, mtandao  huu  jana  ulithibitishiwa  na  mmoja  wa  wanasiasa  wenye  mtandao  mpana  wa  mawasiliano  ndani  na  nje  ya  nchi  kuwa  Profesa  Lipumba  baada  ya  kutua  uwanja  wa  ndege  wa  Rwanda,alisafiri  kwa  njia  ya  barabara  kuelekea  Burundi, ambako  hata  hivyo  haijulikani  yuko  sehemu  gani  na  anafanya  shughuli  gani.



No comments: