Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini Dar es Salaam baada ya kukamatwa jana jioni.
Bado waziri huyo wa zamani ambaye sasa amehamia chama cha upinzani cha Chadema hajasomewa mashitaka yake lakini kwa mujibu wa vyanzo vya polisi, Masha anakabiliwa na kosa la kutumia lugha ya matusi kituo cha polisi.
Masha amefikishwa mahakamani hapo akiwa na vijana wengine 19 ambao wamesomewa shitaka la kutaka kukusanyika bila kibali.
Awali taarifa zinasema Masha alifika katika Kituo cha Polisi cha Osterbay jijini Dar es Salaam jana jioni kwa lengo la kutaka kuwadhamini vijana hao na baadaye alishikiliwa na polisi kituoni hapo.
Masha alikihama Chama cha Mapinduzi hivi karibuni na kujiunga na Chadema na kuteuliwa kugombea Ubunge katika Jimbo la Sengerema katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba.
Mashitaka yanayomkabili waziri huyo wa zamani yanatarajiwa kusomwa baadaye leo mchana.
No comments:
Post a Comment