Dar es Salaam.
Wanafunzi 18,751 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka 2014, wamekosa nafasi ya kujiunga na shule za kidato cha tano kwa sababu mbalimbali ikiwamo ufinyu wa nafasi.
Wanafunzi 18,751 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka 2014, wamekosa nafasi ya kujiunga na shule za kidato cha tano kwa sababu mbalimbali ikiwamo ufinyu wa nafasi.
Kati
ya hao, wanafunzi 479 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi huku
idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo
ikiongezeka kwa asilimia 25 kutoka wanafunzi 117 mwaka 2014 mpaka
kufikia wanafunzi 147 mwaka huu.
“Baadhi ya wanafunzi
wamekosa nafasi kutokana na umri mkubwa na baadhi ya watahiniwa wa
kujitegemea wanakosa sifa za kuchaguliwa,” Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema hapa jana alipokuwa
akitangaza kuchaguliwa kwa wanafunzi hao.
Alisema
wanafunzi 55,003 sawa na asilimia 74.5 ya wanafunzi 73,754 waliofaulu
mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ndiyo waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha tano.
Majaliwa alisema kuna ongezeko la
ufaulu la wanafunzi 918 mwaka huu, ikilinganishwa na wanafunzi 54,085
waliochaguliwa mwaka 2014 kujiunga na kidato cha tano.
Alisema
wanafunzi waliokosa nafasi kuingia kidato cha tano watadahiliwa na
Baraza la Taifa la Ufundi (Nacte) kwenye fani mbalimbali kama vile
ualimu, afya, maendeleo ya jamii na kilimo.
Alisema
ufaulu wa watahiniwa wa kidato cha nne mwaka 2014 kuanzia daraja la
‘distinction’ hadi ‘credit’, yaani ufaulu wa wastani (GPA) wa 5.0 hadi
1.6 ni watahiniwa 73,754 sawa na asilimia 37.4 ya wanafunzi 240,410
waliofanya mtihani huo.
Alisema uchaguzi ulifanyika kwa kufuata machaguo matano ya
tahasusi (combinations) yaliyojazwa na wanafunzi kwenye fomu ya uchaguzi
‘Selform.’
Alisema mfumo wa kompyuta ulitumika katika
kumpanga mwanafunzi katika uchaguzi wake wa masomo na shule kwa kuanzia
na chaguo la kwanza. “Kama mwanafunzi atakuwa hana sifa katika machaguo
yote aliyoomba, hupangiwa chaguo la somo alilofaulu zaidi na katika
shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi kulingana na tahasusi na
nafasi zilizopo,” alisema Majaliwa.
Alisema wanafunzi 29,744 watajiunga na masomo ya sayansi na 25,259 watajiunga na masomo ya sanaa na biashara.
Aliwataka
wanafunzi waliochaguliwa kuripoti katika shule walizopangiwa ili kuanza
muhula wa kwanza wa masomo unaotarajiwa kuanza Julai 18.
“Naagiza
wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati. Endapo
mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya wiki mbili kuanzia tarehe ya
mwisho ya kuripoti, nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine
aliyekosa nafasi,” alisema Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa,
Lindi.
Aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi
wa halmashauri kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kila tarafa kuwa na
shule ya kidato cha tano inatekelezwa kikamilifu ili kuwezesha wanafunzi
wote wanaofaulu kupata nafasi ya kuendelea na masomo. “Wadau wote wa
elimu pia wahakikishe kuwa shule zote zinazoanzishwa kwa ajili ya kidato
cha tano zinakuwa na mabweni kwa kuwa shule hizi ni za kitaifa na
zinapokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini,” alisema.
Kutokana
na kuongezeka kwa ufaulu katika masomo ya sayansi, Majaliwa alihimiza
shule za kidato cha tano zinazoanzishwa kuwa na maabara ili kuongeza
idadi ya wanafunzi wa tahasusi za sayansi na kukidhi mahitaji ya shule
husika.
No comments:
Post a Comment