Membe alonga tuhuma za mabilioni ya Libya - LEKULE

Breaking

1 Jul 2015

Membe alonga tuhuma za mabilioni ya Libya

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameamua kutoa ufafanuzi wa sakata la mabilioni kutoka Libya ambayo amekuwa akihusishwa nayo, akieleza kuwa fedha zote zilizotolewa kwa amri ya mahakama ni mkopo na hazikuchotwa kama ilivyokuwa kwenye kashfa za Epa au Escrow.
Membe amekuwa akihusishwa na fedha hizo, Dola 20 milioni za Marekani (sawa na Sh40 bilioni) ambazo zilikuwa zimehifadhiwa katika akaunti ya Libya No.004-200-0002216-01 iliyokuwa Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB).
Kwa mujibu wa waraka alioutoa jana kwa vyombo vya habari kuhusu fedha hizo, Membe alisema Serikali ya Libya na Tanzania zilitia sahihi mkataba wa nyongeza (Addendum to the Dept Swap Agreement) ambao ulizungumzia, pamoja na mambo mengine, matumizi ya fedha hizo.
Mkataba huo wa nyongeza unatamka katika kifungu No.4.02, kwamba, fedha hizo zikopeshwe kwa mwekezaji aliyeteuliwa na Libya, ambaye ni kampuni ya Meis Industries Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Saruji mkoani Lindi.
“Ni mkopo uliotolewa kwa Kampuni ya Meis kwa mujibu wa Mkataba wa Makubaliano (Investment Agreement) wenye masharti ya kibenki. Na Masharti hayo ya kibenki yanamtaka mwekezaji kuweka dhamana, kulipia riba, kuwekewa muda wa kurudisha mkopo, na anawekewa hatua za kuchukuliwa endapo mwekezaji huyo atashindwa kulipa mkopo,” anaeleza Membe.
“Kwa lugha nyingine, kampuni ya Meis ikishindwa kulipa mkopo huo, itafilisiwa mali zake na TIB itarudishiwa fedha zake. Iacheni benki ifanye kazi yake. Mkopo unageukaje kuwa ufisadi?”
Membe alisema yeye hana kampuni hapa nchini, hana ubia na kampuni yoyote, pia hana hisa katika kampuni ya Meis na hajafaidika na mkopo huo ambao unasimamiwa na TIB.
“Ndiyo maana uvumi kuwa nahusika na ufisadi wa mabilioni ya Libya hauna mashiko kabisa. Baadhi ya wanasiasa wenzangu wanajua ukweli wote huu, lakini kwa makusudi wanaamua kuwafanya watu waamini,” anasema Membe kwenye waraka huo.
Anasema ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Lindi unaendelea vizuri na mitambo yote inayotakiwa katika ujenzi huo imeshawasili.
“Asilimia 45 ya ujenzi wa kiwanda hicho umekamilika na ni mategemeo ya kampuni ya Meis kuwa kiwanda hicho kitakamilika ifikapo Desemba mwaka huu wa 2015,” anasema.
Alisema kumbukumbu zinaonyesha mambo mawili, kwamba, kabla ya Serikali ya Libya kutia sahihi nyongeza hiyo ya mkataba iliyotaka fedha zikopeshwe kwa Meis, upembuzi yakinifu wa mradi husika ulifanywa na Libya kupitia vyombo vyake, walishajiridhisha juu ya ubora wa mradi huo.
Pili alisema baada ya kutia sahihi nyongeza ya mkataba, serikali ya Libya kupitia ubalozi wake hapa nchini iliendelea kusisitiza kwa maandishi kwamba Serikali ya Tanzania iharakishe mchakato wa kuwezesha fedha hizo zikopeshwe kwa mwekezaji waliyemteua ili mradi huo muhimu usiendelee kuchelewa, na pia fedha ziingie katika mzunguko kwa manufaa ya Watanzania.
“Katika kutekeleza mikataba hii miwili, yaani na kwa kuzingatia umuhimu ambao Serikali ya Libya iliuonyesha, Serikali ya Tanzania kupitia watalaamu wake wa Wizara ya Fedha, TIB, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Meis, walikutana chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na kuandaa hadidu za rejea ambazo zilisababisha kutengenezwa kwa mkataba wa uwekezaji kati ya serikali ya Tanzania, TIB, Serikali ya Libya na Mwekezaji,” alisema.
“Serikali ya Tanzania, TIB na mwekezaji walitia sahihi mkataba huu na kuupeleka Libya ili serikali ipate kuweka sahihi, lakini kwa sababu ambazo hazikufahamika, serikali ya Libya haikutia sahihi mkataba huo.”
Kutokana na hilo, Membe alisema Septemba 13, 2010 mwekezaji alifungua shauri la madai No. 124/2010 Mahakama Kuu ya Tanzania, dhidi ya Libya, akiiomba Mahakama Kuu itoe tamko kwamba kitendo cha Libya kukataa kutia sahihi mkataba huo hakikuwa cha haki na kwamba mahakama itoe amri kwamba fedha hizo zitolewe kwa mwekezaji ili kutekeleza mradi uliokusudiwa.
“Kumbukumbu zinaonyesha kwamba wito wa mahakama (summons) ulipelekwa ubalozi wa Libya, lakini hapakuwa na majibu wala mwakilishi aliyekuja mahakamani,” alisema.
Alisema Mahakama Kuu, kwa kufuata taratibu zake, iliendelea kusikiliza shauri na kutoa amri kama ambavyo mahakama yenyewe ilijiridhisha. Amri ya mahakama, pamoja na mambo mengine, iliagiza kwamba fedha hizo zitolewe kwa mwekezaji ili kutekeleza mradi husika.
Alisema TIB, AG walipinga hilo lisitekelezwe lakini mwisho wa yote maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa katika mchakato mzima yakawa kwamba Meis ilikuwa na haki ya kupewa fedha za mradi wa kiwanda hicho cha saruji kama ilivyoanishwa katika mkataba kati ya Serikali na Libya.
“Ni dhahiri kwamba, mgogoro huu ulichujwa na mahakama mpaka ngazi ya juu kabisa, tena kwa nyakati tofauti na mbele ya waheshimiwa majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa,” alisema Membe katika taarifa yake.
“Katika Taifa linaloongozwa kikatiba, chini ya utawala wa sheria kama Tanzania, ambako Mahakama ndicho chombo kilichopewa mamlaka ya mwisho kuamua juu ya haki za raia na hata serikali, si rahisi na wala haitakuwa sahihi kwa mtu yeyote kuhoji uhalali wa mchakato huu kama ulivyoongozwa, kuelekezwa na kuamuliwa na mahakama, isipokuwa tu kama sheria inatoa mwanya mwingine kurudi mahakamani kwa mtu yeyote ambaye hajaridhika au anayetaka kuhoji maamuzi haya kwa namna yoyote.
“Mahakama iliamua kwa mujibu wa sheria. Na kwa kuwa hakuna aliyeendelea kupinga kimahakama, suala hili lichukuliwe kwamba limefikia mwisho na limefungwa.”

No comments: