Ukawa hakijaeleweka - LEKULE

Breaking

15 Jul 2015

Ukawa hakijaeleweka

Dar es Salaam.
Mambo yamekuwa mazito. Ndivyo inavyoonekana baada ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushindwa kutangaza mgombea urais jana badala yake ukatoa ahadi mpya kwamba sasa atatangazwa muda wowote ndani ya siku saba.

Kauli hiyo inayoibua maswali mengi imekuja baada ya viongozi wa umoja huo waliofanya vikao hadi usiku jana bila ya viongozi wakuu wa CUF ambao wameahidi kutoa msimamo wao leo saa 5.00 asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho kilichodumu kwa saa 11.30, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema wamekamilisha mazungumzo ya kumpata mgombea wa urais ambaye watamtangaza kwenye mkutano wa hadhara muda wowote ndani ya siku saba.

Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi akizungumza akiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi na viongozi wengine wa vyama hivyo alisema hakuna mpasuko kama inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF katika umoja huo.

Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na naibu wake wa Bara, Magdalena Sakaya hawakuhudhuria kikao hicho kilichofanyika kuanzia saa 4.00 asubuhi kwenye Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

Badala yake, Sakaya aliiambia Mwananchi jana jioni kuwa CUF haikuweza kushiriki kikao hicho kwa kuwa kulikuwa na mambo ambayo hawajakubaliana ndani ya chama na kwamba kama wangemaliza mapema, wangekwenda kwenye kikao hicho.
Baadaye usiku, CUF ilituma taarifa kwa vyombo vya habari ikisema kuwa itazungumza na waandishi wa habari leo saa 5.00 asubuhi kwenye ofisi za chama hicho Dar es Salaam kutoa taarifa kuhusu Ukawa.

Kutokuwapo kwa viongozi wa CUF jana na habari kwamba chama hicho kitatoa taarifa peke yake leo, kunaweka giza nene mbele ya vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD, ambavyo vilikubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
Kutokuwapo kwa viongozi wa CUF kulisababisha Ukawa kushindwa kumtaja mgombea wake na habari ambazo zilipatikana awali, zilisema huenda vyama hivyo vikatangaza jina la chama kitakachotoa mgombea urais badala ya jina la mgombea.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema hoja kubwa ilikuwa katika suala la mgombea urais, nafasi ambayo inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye ameshachukua fomu za CUF na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye anaungwa mkono na vyama vyote vinne.
Tayari Profesa Lipumba ameshagombea urais mara nne bila ya mafanikio, wakati Dk Slaa aligombea mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili, akiwa ameitikisa CCM iliyopoteza asilimia takriban 20 ya kura za mwaka 2005.

Sakaya alisema jana kuwa CUF haikushiriki kikao cha jana kutokana na kutoafikiana baadhi ya mambo ndani ya chama chake, ikiwa ni pamoja na suala hilo la kusimamisha mgombea mmoja wa urais kupitia Ukawa.

“Nilimpigia simu (naibu katibu mkuu wa Chadema, John) Mnyika kumwambia kwamba tunaweza tukachelewa kwa sababu tulikuwa katika kikao cha CUF cha majadiliano, lakini mpaka sasa (saa 1:48 usiku) bado hatujapata mwafaka,” alisema Sakaya na kuongeza:

“Tukishakamilisha majadiliano yetu kama chama, tutakwenda kuzungumza chini ya mwamvuli wa Ukawa kwa sababu tunahitaji kujiridhisha kwanza kabla ya kuzungumza au kufanya maamuzi yoyote.” alisema.
Sakaya alipoulizwa ni mambo gani ambayo hawajakubaliana na wenzao wa Ukawa, alisema hawezi kuyazungumza hadi pale watakapoyamaliza na kuwaita wanahabari kwa pamoja na kutoa ufafanuzi.
Alisema hawakutuma mwakilishi katika kikao hicho na kwamba kama kulikuwa na mwakilishi aliyekwenda kwa ajili yake binafsi na si kukiwakilisha chama.

Viongozi wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD vinavyounda umoja huo, walianza kuingia kwenye ukumbi wa hoteli hiyo saa 3.00 asubuhi, huku Dk Slaa akiwaeleza waandishi wa habari kwamba hoja kubwa ya kikao hicho ilikuwa ni mgawanyo wa majimbo, yakiwamo 26 mapya pamoja na kumtaja mgombea urais.

“Tutawaeleza kinachoendelea ngoja tuingie katika kikao kwanza. Ila hoja kuu ndiyo hizo mbili na tukishakubaliana tutawaeleza wala haina shida,” alisema Dk Slaa.

Takriban wiki moja iliyopita, Profesa Lipumba akiwa na viongozi wakuu wa Ukawa waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa mgombea urais wa Ukawa angetangazwa Julai 14 (jana), kwa maelezo kuwa majadiliano yalikuwa yakiendelea.

Lakini jana, Profesa Lipumba pamoja na viongozi wenzake wa CUF, hawakuonekana, jambo ambalo liliibua maswali mengi kwa wanahabari.

Katika kuonyesha kuwa kikao hicho kilipangwa kuwa siri, viongozi wa Ukawa hawakutaka kutaja eneo kinapofanyika na kuwaeleza wanahabari kuwa wataitwa kupewa taarifa na kufafanua kuwa kulikuwa na vikao vya ndani vilivyokuwa vikiendelea.

Hata baada ya wanahabari kubaini eneo ambalo kikao hicho kinafanyika, viongozi hao walikuwa wagumu kutoa taarifa.

Habari kutoka kwa viongozi wa vyama hivyo zinasema kuwa Profesa Lipumba anashinikiza kupitishwa na Ukawa kugombea urais, jambo ambalo linapingwa na viongozi wengine wa vyama vinavyounda umoja huo kwa maelezo kuwa tayari CUF imesimamisha mgombea wa urais Zanzibar.

Idadi kubwa ya viongozi wa vyama hivyo wanashinikiza Dk Slaa apewe nafasi hiyo kutokana na kukubalika zaidi kuliko Profesa Lipumba. Pia anapigiwa upatu kutokana na rekodi yake kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 wakati alipomtikisa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa hoja ya ugawaji wa majimbo haikuwa na nguvu kama ya urais ambayo imekitikisa kikao cha jana mpaka kufikia hatua ya viongozi kulumbana waziwazi na kuonyana kwamba wasipokuwa makini umoja huo utatetereka.

“Leo viongozi wa CUF hawapo, wapo wa vyama vingine,” alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo na alipotakiwa kufafanua sababu hiyo alisisitiza kusema kwamba “hata kwa macho huoni kaka”.

Awali, licha kutokuwapo kwa wawakilishi wa CUF, viongozi wengine wa umoja huo walishindwa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari saa 9.30 alasiri kama walivyokuwa wameahidi badala yake walimtuma Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene kuwaeleza wanahabari kuwa mjadala uliokuwa ukiendelea ulikuwa wa majimbo mapya kwa kuwa ni suala jipya na lilikuwa limeibua changamoto mpya.

“Kwa sasa viongozi wanajadili kuhusu majimbo mapya ya uchaguzi ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeyatangaza juzi. Subirini tu wala msiwe na haraka,” alisema Makene na kuahidi kuwa taarifa za kikao zingetolewa saa 12.30 jioni.

Hata ulipofika muda huo, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa zaidi ya waandishi wa habari kutakiwa kuvuta subira mpaka kikao kimalizike. Ilipofika saa 1.45 usiku, Makene aliwaeleza waandishi wa habari kwamba majadiliano bado yalikuwa yakiendelea na muda wowote taarifa zingetolewa.

Viongozi wengine waliokuwapo katika kikao hicho ni Mnyika, Dk Slaa na Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe.

Mtatiro aonya kuvunjika

Akiandika katika ukurasa wake wa Facebook, naibu katibu mkuu wa zamani wa CUF, Julius Mtatiro jana aliwaonya wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa wanaosema “bora Ukawa ivunjike”, akisema hali hiyo ikitokea vyama hivyo havitabaki salama.

Mtatiro, ambaye amekiri kuandika onyo hilo kwenye ukurasa wake, alisema: “Mimi nataka kurudia kusema hapa, kwamba Ukawa ikivunjika kwa sababu yoyote ile, ni kitendo cha vyama vya upinzani kuwasaliti wananchi. Hakuna lugha nyingine.”

Alisema wanaofurahia Ukawa kutetereka na wanaoombea ivunjike wanafanya maombi yasiyo na tija kwa Taifa, kwa kuwa Ukawa ikishavunjika vyama vya upinzani havitabaki salama hata kidogo.

“Athari ambazo chama kimoja kimoja kinazipata ndani ya Ukawa ni chache kuliko chama kimoja kikienda kivyake,” alisema.

“Ukawa ilikuwa na malengo makubwa sana. Ukiachilia mbali uchaguzi, kuna ajenda ya Katiba. Tuliondoka kwenye Bunge la Katiba na kuacha Sh. 30 milioni kila mjumbe kwa sababu ya kujenga mshikamano wa upinzani. Kuvunja Ukawa leo ni kusema pia tunakubali Katiba Inayopendekezwa.”

No comments: