Dk Magufuli: Sitaogopa mtu yeyote - LEKULE

Breaking

15 Jul 2015

Dk Magufuli: Sitaogopa mtu yeyote

Dar es Salaam.
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema akichaguliwa kuwa rais, hatamwogopa mtu wala hataacha mtu aonewe, hasa wanyonge.

Dk Magufuli alikuwa akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Zakhem, Mbagala.

Katika mkutano huo ulioandaliwa CCM mkoani Dar es Salaam, Dk Magufuli alikuwa akitoa angalizo kila mara kuwa hawezi kuzungumza sana kwa kuwa wakati wa kampeni haujafika, ingawa katika hotuba yake fupi alitoa ahadi mbalimbali zenye sura ya kampeni.

Aliahidi kuwa atawashughulikia watendaji wa Serikali ambao ni wazembe na kuhimiza utekelezaji wa ilani ya CCM. Aliongeza kuwa hatamwonea haya mtu yeyote atakayekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Taifa.

“Mimi siyo mkali, mimi ni mtu mpole sana lakini nawachukia watendaji wa Serikali ambao ni wazembe, na hao ndiyo nitakao lala nao mbele,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliohudhuria mkutano huo.

Dk Magufuli alisisitiza kuwa atasimamia ilani ya chama ambayo imezingatia masuala ya kilimo na biashara. Alisema ilani inawalinda wafanyabiashara wadogo na wakubwa, pia kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

“Maendeleo hayana chama lakini maendeleo ya kweli yataletwa na CCM. Wakati wa uchaguzi ukifika mchague wabunge na madiwani wa CCM ili kukamilisha mafiga matatu,” alisema Magufuli.
“Ukiwa na tochi inayotumia betri tatu, wewe ukaweka betri mbili halafu katikati ukaweka gunzi, hiyo tochi itawaka?” Dk Magufuli aliuliza makutano ambao nao walimjibu kwa pamoja “haiwaki”.

Dk Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, aliwashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata kuanzia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) hadi viwanja vya Zakhem, Mbagala.

Alisema yeye na mgombea mwenza watahakikisha wanalipa fadhila kwa vitendo, endapo watashinda Uchaguzi Mkuu ujao na kuongoza Serikali.
“Ninawashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kuweka pembeni kambi zenu na kujitokeza kutupokea wagombea wenu. Tulikuwa wagombea 42 wenye sifa sawa, na kila mmoja alikuwa na kambi yake. Kuwa na kambi siyo kosa. Lakini wote wamevunja kambi zao na kuniunga mkono ili kukipa ushindi Chama cha Mapinduzi,” alisema.

Alisema alipokwenda kuchukua fomu, wakati anatafuta wadhamini na wakati anarudisha fomu alikuwa akiwaambia waandishi wa habari neno moja tu; “Watanzania mniombee”.

Aliwashukuru wananchi kwa kumwombea na kusema Mungu amejibu maombi yao ndiyo maana amechaguliwa kuiwakilisha CCM kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
“Nilipokuwa Dodoma nilisema tutahakikisha tunasimamia haki na maendeleo kwa Watanzania wote. Ninaomba wananchi mkiamini Chama cha Mapinduzi, uchaguzi ukifika mchague rais, wabunge na madiwani wa CCM,” alisema.

Awali, akimkaribisha mgombea huyo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais tayari, sasa wanaanza mchakato wa kuwapata wagombea ubunge na udiwani.

“Tumemaliza mchakato wa urais, sasa tunageukia ubunge na udiwani. Chama chetu kimekomaa kidemokrasia, tutatenda haki kwa wagombea watakaojitokea kuwania nafasi hizo. Ninawahakikishia kuwa chama chetu ni makini na tutashinda kwenye uchaguzi ujao,” alisema Kinana.

Asifu mapokezi 

Dk Magufuli aliwasili kwenye viwanja hivyo saa 8:20 mchana na kuondoka saa 9:50 baada ya hotuba fupi.  Mabasi ya Uda na daladala yakiwa yamepakia wafuasi wa CCM yalianza kufika kwenye viwanja hivyo tangu saa 6:00 mchana na ilipofika saa 8:00 mchana, uwanja huo ulifurika na kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi.
Saa 8:10 mchana, msafara wa pikipiki zaidi ya sitini zilizokuwa zikiendeshwa na vijana, uliingia kwenye viwanja hivyo ukitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kufanya mamia ya watu waliuokuwa kwenye viwanja hivyo kusimama kumpokea huku wakishangilia na kuimba wakiongozwa na bendi ya TOT.

 Magufuli hodari wa ngoma

Baada ya kumaliza kuhutubia, Dk Magufuli alipanda kwenye jukwaa la wanamuziki wa TOT na kupiga tumba huku akicheza na kuwa kivutio katika uwanja huo.

 Foleni.

Tangu saa 7:00 mchana hadi jioni kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari kwenye Barabara ya Kilwa uliotokana na ugeni huo.
Baadhi ya watu walionekana wakitembea kwa miguu baada ya daladala walizopanda kukwama kwenye foleni.

No comments: