Dar es Salaam.
Siku moja baada ya watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kuvamia kituo cha Polisi Stakishari kuua na kupora silaha, mmoja wa walionusurika katika tukio hilo askari Gaston Shadrack amesimulia hali ilivyokuwa.
Siku moja baada ya watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kuvamia kituo cha Polisi Stakishari kuua na kupora silaha, mmoja wa walionusurika katika tukio hilo askari Gaston Shadrack amesimulia hali ilivyokuwa.
Askari huyo
aliyejeruhiwa bega la kulia na kifua kwenye uvamizi huo juzi usiku
alisema alikuwa kwenye lindo kituoni hapo kabla ya wanaume wanane kufika
na kudai wamedhulumiana.
“Ilikuwa saa 4 kuelekea saa 5
usiku. Lilikuja kundi la wanaume wanane wakiwa wamevaa makoti makubwa
lakini hawajafunika nyuso. Walikuwa wakilalamika, “haiwezekani
unidhulumu’ huku wakielekea ndani ya kituo.”
Aliongeza
kuwa: “Utaratibu wetu ni lazima mtu akifika apite getini kwa mlinzi kwa
ajili ya kupewa maelekezo ili aende ndani. Ila wao walitaka kwenda moja
kwa moja,” alisimulia Shadrack ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili (MNH).
Kutokana na utaratibu huo wa
kuanzia getini, aliwaita watu hao kwa ajili ya kupata maelekezo ya
kwenda ndani. Wakati huo akiwa na askari wenzake wanne hapo nje.
“…Kitendo
cha kuwaita na kuwauliza mnakwenda wapi, wale jamaa waligeuka na kuvua
makoti kumbe ndani walikuwa na bunduki. Wakaanza kutushambulia mimi na
askari wenzangu ambao walianguka chini huku wengine wakifyatua risasi
juu, nikageuka haraka na kulalia tumbo lakini wakati nageuka jambazi
mmoja alinipiga risasi ikanipata kwenye bega la kulia na kifuani,”
alisema Shadrack huku akionyesha majeraha hayo.
Alisema baada ya hapo majambazi hao waliingia kituoni na kuendelea kufyatua risasi lakini mmoja wao alibaki nje ya kituo.
“Nilitumia mwanya huo kunyanyua bunduki niliyokuwa nayo na kumfyatulia risasi akandondoka na mimi nikakimbia.”
Polisi kuzikwa na mama yake
Katika hatua nyingine, mmoja kati ya askari polisi wanne
waliouawa katika tukio hilo, atazikwa siku moja na mama yake ambaye
alifariki dunia baada ya kusikia kifo cha mwanaye, Koplo Gaudin.
Akizungumza
na Mwananchi, Mkuu wa Polisi Ukonga, Mrakibu Mwandamizi, Jiliyo Simba
alisema, mama wa askari huyo, alipoteza maisha baada ya kupokea habari
za msiba wa mwanaye.
“Mama wa Koplo Gaudin alikuwa mgonjwa na alipopokea taarifa za kifo cha mwanaye naye alifariki dunia,” alisema.
Alibainisha
kuwa kutokana na hali hiyo amehimiza uchunguzi wa mwili wake
(postmorterm) kufanyika jana ili uandaliwe kwa ajili ya safari kwenda
Karagwe na mazishi yawe leo kijijini kwao, wilayani Karagwe.
Alisema
miili ya askari wengine (mikoa wanayotoka ikiwa katika mabano)
itasafirishwa leo kwa maziko ni pamoja na Sajenti Adam (Mara), askari
mpelelezi, Kapteni Peter (Geita) na Konstebo Anthony atakayezikwa mkoani
Kilimanjaro.
Mbunge wa Jimbo la Segerea, Makongoro
Mahanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, ametoa
salamu za rambirambi akisema, tukio hilo ni kubwa na siyo la kawaida
hivyo kuna haja ya Serikai kulipa uzito wa pekee.
“Huu ni wizi wa silaha kwa ajili ya kwenda kufanyia ujambazi, kama siyo hivyo, wangevunja selo kuwanasua wenzao,” alisema.
Wakati huohuo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imelaani vikali mauaji ya raia na askari polisi hao tena wakiwa kazini.
Mwenyekiti
wa THBUB, Bahame Nyanduga kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya
habari alisema: “Tume inaiomba Serikali kuyapa umuhimu wa kipekee
matukio haya kwa kufanya uchunguzi wa kina ili kupata majawabu sahihi ya
kudhibitiwa mapema na kuwahakikishia askari usalama wao.”
No comments:
Post a Comment