Ugaidi unavyopenya Tanzania - LEKULE

Breaking

15 Jul 2015

Ugaidi unavyopenya Tanzania

Dar es Salaam.
Tukio la kwanza lenye sura ya kigaidi lilitokea Dar es Salaam mwaka 1998 na la hivi karibuni limetokea katika cha Polisi cha Sitakishari, Ukonga ambako watu wasiojulikana walivamia na kuua askari wanne na raia watatu na kisha wakapora silaha.
Shambulio la kigaidi la Agosti 1998 lilisimamiwa na Mtanzania na lilisababisha vifo vya watu 11 kwenye jengo la ofisi za ubalozi wa Marekani nchini. Tangu wakati huo kumekuwa na ushiriki wa kutisha wa Watanzania katika uhalifu wa kutumia nguvu.
Matukio ya siku za karibuni yanafanana. Watu wasiojulikana huvamia vituo vya polisi, kuua askari na kupora silaha. Hawaibi kitu kingine chochote isipokuwa silaha. Walifanya hivyo Ikwiriri wilayani Rufiji, Kimanzichana wilayani Mkuranga, Bukombe wilayani Bukombe, Geita mkoani Geita na Amboni mkoani Tanga ambako watu waliojihami kwa bunduki walirushiana risasi na kujeruhi askari sita.

Historia

Duniani matukio ya kigaidi yana historia ndefu. Kuna wakati Serikali ndizo zilikuwa zinafanya ugaidi kwa kufanya mauaji au kutoa vitisho kulazimisha utiifu wa wananchi, lakini baadaye vitendo hivyo vikawa vinatumiwa na makundi ya wahalifu kushinikiza madai ya kisiasa au kidini kama yanavyofanya makundi kama Al Qaeda lililotapakaa ulimwenguni, Boko Haram la Nigeria na Al Shabab la Somalia. Lakini Islamic State limehusisha utekaji wa maeneo ya kiutawala.

Matukio ya kigaidi yamerekodiwa tangu karne ya kwanza, lakini shambulio lililofanywa na kikundi cha kigaidi cha Black September Organization mwaka 1972 na kuua wanamichezo 11 wa Israeli waliokwenda kushiriki Michezo ya Olimpiki jijini Munich, Ujerumani ndilo liliifanya dunia ishtuke na kuanza kuchukua hadhari.

Shambulio hilo lilipangwa na kutekelezwa na magaidi wa Kipalestina ili watangazwe na dunia ijue madai yao. Ingawa wachezaji wa Israel ndiyo waliokumbwa na mkasa ule, magaidi walitaka watambuliwe na watazamaji televisheni wapatao bilioni moja.

Shambulio jingine kubwa ni lililofanyika Oktoba 1983, Mashariki na Kati magaidi walipolipua kikosi cha jeshi la majini la Marekani kilipokuwa kinawasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Beirut. Wanajeshi 241 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa. Miongoni mwa mashambulizi ya kigaidi ambayo Marekani haitasahau ni la Septemba 11, 2001 ambapo majengo pacha ya biashara WTC, makao makuu ya jeshi (Pentagon) yalishambuliwa.

Vikundi vya kigaidi

Vipo vikundi vingi vya kigaidi na asilimia zaidi ya 90 vikiwa katika nchi za Mashariki ya Kati. Pia, vipo vichache maarufu ni kama Red Brigade cha Italia, ETA cha Hispania, Japanese Red Army. Gaidi maarufu katika miaka ya 2000 alikuwa Osama bin Laden, lakini aliyetikisa dunia miaka ya 1970 hadi 1990 alikuwa Ilich Ramírez Sánchez wa Venezuela maarufu kama Carlos The Jackal.

Tanzania

Nchi zote tatu za Afrika Mashariki zimekumbwa na mashambulizi ya kigaidi kwa nyakati tofauti. Shambulio la kwanza lilifanywa Agosti 1998 katika balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya.
Kenya imeathirika zaidi; ilishuhudia mashambulizi kwenye Hoteli ya Nrofilk (1998), Hoteli ya Paradise (2002), jengo la Westgate (2013), Mpeketoni (2014) na Chuo Kikuu cha Garisa (2015). Nchini Uganda, mashabiki walishambuliwa wakati walipokuwa wanatazama fainali ya Kombe la Dunia (Julai 2010), na pia basi la abiria lililokuwa linakwenda Nairobi.

Ushiriki wa Watanzania katika matukio ya kutisha, kujeruhi, kuua, kupora silaha, kulipua mabomu na kupambana na askari yamekuwa yakiongezeka. Hata hivyo, Serikali haijaeleza wala kuthibitisha uwapo wa magaidi nchini.

Novemba 2011: Serikali ya Tanzania ilitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi baada ya Watanzania 10 kukamatwa wakati wakivuka mpaka wa Kenya-Somalia kwenda kujiunga na kundi la al Shabab.

Juni 2012 alikamatwa raia mmoja wa Ujerumani kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kujiunga na kundi la al Shabab.

Oktoba 2012 polisi mmoja alishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana kwa panga Zanzibar.

Oktoba 2012 makanisa sita yalichomwa moto jijini Dar es Salaam kwa siku moja eneo la Mbagala wilayani Temeke

Novemba 2012 lilifanyika shambulio dhidi ya imam mmoja mwenye msimamo wa wastani visiwani Zanzibar.

Desemba 2012 Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mpendae Zanzibar alipigwa risasi wakati anafungua geti ili aweze kuingia nyumbani kwake eneo la Kitomondo.

Februari 2013 Mchungaji wa Kanisa la Pentecoste Assemblies of God Tanzania (PAGT) Buseresere, wilaya ya Chato, Mathayo Kachila (45) aliuawa katika mzozo wa nani mwenye haki ya kuchinja kati ya Waislamu na Wakristo.

Februari 2013 Padri wa Kanisa Katoliki Minara Miwili Zanzibar, Evarist Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi.

Mei 2013 Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Olasiti lilishambuliwa na mfanyakazi jijini Arusha alipigwa bomu; watu watatu walifariki na wengine 63 kujeruhiwa.

Aprili 2015: Mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Bihawana, Dodoma alikamatwa kwa kuhusika na mauaji ya kigaidi kwenye Chuo Kikuu cha Garissa.

Aprili 2015: Wasichana watatu, akiwamo Mtanzania walikamatwa mpakani mwa Kenya na Somalia wakati wakienda kujiunga na kundi la al –Shabab kuwatumikia kingono.

Matukio hayo yote yanatoa picha kuwa kuna ugaidi unajipenyeza taratibu nchini.

No comments: