Uchaguzi
wa kura za maoni ndani ya Chadema katika Jimbo la Bariadi umeahirishwa
baada ya kubainika kwa matukio yanayoashiria vitendo vya rushwa.
Wakizungumza
baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo, wajumbe wa mkutano mkuu wa
wilaya walisema hawataki kuingiliwa na virusi vya rushwa ndani ya chama
hicho, kwa kuwa hali hiyo italeta mpasuko na makundi.
Wajumbe
hao wameutaka uongozi Chadema kuwa makini na wanachama mamluki
wanaohama kutoka vyama vingine vya upinzani ili wasikivuruge.
“Hatua
ya kuahirishwa kwa uchaguzi inaonyesha ni namna gani chama kilivyo
makini ili wanaotoa rushwa wajifunze umakini huu na wananchi waelewe
kuwa chama kinatetea wanyonge,” alisema Makula Saguda.
Hata
hivyo, mjumbe mwingine, Masanja Lujani alipinga hatua hiyo akisema
kuahirishwa uchaguzi ni ubadhilifu ambao haufai akisisitiza kuwa kama
wamekamata mtu akiwa anagawa rushwa wangemtoa katika uchaguzi na wengine
wakaendelea.
Msimamizi
wa uchaguzi huo, Emmanuel Mbise alisema uchaguzi huo umeahirishwa baada
ya kukamata watu wakigawa rushwa kwa baadhi ya wagombea.
“Chadema
kinaaminiwa na kinapendwa na watu kwa sababu hakikubaliani na rushwa,
kwa mujibu wa katiba na mamlaka niliyopewa, nimeamua kuahirisha uchaguzi
hadi utakapotangazwa tena kutokana na uchaguzi huu kutawaliwa na
rushwa,” alisema Mbise.
Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Wilson Mshuda ambaye pia ni mgombea katika
jimbo hilo alisema: “Hatuwezi kunyamaza kimya, hata katiba ya chama
kuanzia ukurasa wa 86 inaongelea mgombea ambaye ataonekana kutoa rushwa kwa wajumbe kuwa atakuwa amejiondoa katika kinyang’anyiro.”
Jimbo
la Bariadi lina wagombea 12 ambao ni Godwin Simba, Mshuda, Masanja
Madoshi, Seni Silanga, Manyangu Kulemwa, Zacharia Shigukulu, Maendeleo
Makoye, Sweya Makungu, Sitta Mulomo, Wilson Limbu, Slivatus Masanja na
Ntemi Ndamo.
No comments:
Post a Comment