ALIYEKUWA
Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Bi.Esta Bulaya ambaye juzi alitangaza kujiunga na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amepata mapokezi makubwa Mjini Bunda
jana akitokea jijini Mwanza akiwa na viongozi wa CHADEMA mkoani humo na
Kanda ya Ziwa.
Akiwahutubia
wananchi katika Viwanja vya Stendi ya Zamani, Bi.Bulaya aliwapongeza
wananchi kwa mapokezi makubwa waliyompa na kumlipua mbunge wa jimbo hilo
aliyemaliza muda wake, Bw. Stephen Wassira akisema muda wake wa kukaa
serikalini unatosha.
Alisema
katika Serikali ya Awamu ya Tano, viongozi kama Bw. Wassira hawafai
kwani amekuwa Waziri muda mrefu lakini jimbo hilo bado halina maendeleo
yaliyotarajiwa na wananchi.
"Wazazi
wangu mimi ni mwanachama wa CCM na mimi nimekulia ndani ya chama hicho
hivyo mkiona nimekimbia, mjue mambo yamenifika shingoni, katika mkoa huu
kuna rasilimali nyingi ambazo hazijatumika vizuri ili ziwaondolee
wananchi umaskini," alisema.
Akizungumzia
uwazi na uwajibikaji, alisema viongozi wengi wa CCM hawataki kuwatetea
wananchi na kushindwa kuwasimamia watendaji wa Serikali akitolea mfano
mradi mkubwa wa maji mjini humo ambao umechukua miaka tisa bila
Bw.Wassira kuukamilisha.
"Leo
hii Wassira atakuja na sera gani kwa wananchi wakati ameshindwa
kutekeleza wajibu wake kama mbunge na kiongozi wa Serikali, tuwakatae
viongozi wa ngazi zote wanaotokana na CCM," alisema.
Aliongeza
kuwa, umefika wakati wa majimbo yote mkoani humo kuchukuliwa na
wagombea wa CHADEMA ambao watatimiza ahadi zao kwa wananchi na kutatua
kero walizonazo.
Bi.Bulaya
aliweka wazi dhamira yake ya kuwania ubunge wa Bunda Mjini kwa tiketi
ya CHADEMA ambapo leo atashiriki kura ya maoni ya kumpata mgombea ubunge
wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA.
Naye
mbunge wa Kahama, Bw. James Lembeli, alidai kuchoshwa na ufisadi uliopo
ndani ya CCM na kuwataka wananchi wakubali kuiunga mkono CHADEMA kwa
kuwaweka madarakani na kushika dola katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25,
mwaka huu.
Mbunge
wa Musoma Mjini, Bw. Vicent Nyerere, alilitaka Jeshi la Polisi kutoa
ushirikiano katika Uchaguzi Mkuu na kuacha kuitetea CCM huku akidai
jeshi hilo ni sehemu ya Watanzania ambao wote wamepigika.
No comments:
Post a Comment